Watumishi wa Serikali Wizara ya Maliasili na Utalii
wametakiwa kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii na
kujiepusha na vitendo vya rushwa kuhakikisha jukumu kuu la Wizara hiyo
linafikiwa ambalo ni kuendeleza Uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza
Utalii nchini.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Maj.
Gen. Gaudence Milanzi akifungua Mkutano wa 23 wa Baraza la Wafanyakazi
uliofanyika jana katika Chuo cha Taifa cha Utalii, tawi la Bustani, Jijini Dar
es Salaam.
Alisema kuwa kila mtumishi katika nafasi yake anatakiwa
kuwa mbunifu, kuongeza maarifa katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo na
kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
Amewataka pia watumishi hao kuwa waadilifu, kufanya kazi
kwa ushirikiano na kujiepusha na makundi yasiyokuwa na tija kwa Wizara na
Serikali kwa ujumla.
Alionya kuwa, Mtumishi yeyote atakeenda kinyume cha
sheria na taratibu hatosita kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kuachishwa
kazi ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ya
"HAPA KAZI TU"
“Mtumishi ambaye hatakua pamoja na sisi katika kutii
sheria, kanuni na taratibu kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na ujangili
tutamuondoa” Alisema Maj. Gen. Milanzi.
Amesema imekuepo tabia ya baadhi ya watumishi kujihusisha
na vitendo vya rushwa na wengine kushiriki kwenye matukio ya Ujangili jambo
ambalo linaipatia Wizara sifa mbaya. Alisisitiza kuwa vitendo kama hivyo kwenye
Serikali ya awamu ya tano havitakuwa na nafasi.
Wakizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika
kutekeleza majukumu yao ipasavyo, watumishi wa Maliasili waliopata fursa ya
kuchangia walisema changamoto kubwa ni uhaba wa fedha na vitendea kazi muhimu
hususani kwa wale wanaohudumia Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu.
Maj. Gen. Milanzi alimuwakilisha Waziri wa Wizara ya
Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ambaye yupo kwenye majukumu mengine
ya Kiserikali Mkoani Dodoma.
Hamza Temba - Afisa Habari
Wizara ya Maliasili na Utalii
0713 635204
0785 798011
No comments:
Post a Comment