Tuesday, February 16, 2016

WAMILIKI WA GOLDEN TULIP WAKUBALIANA NA SERIKALI

Na Mwandishi Wetu

Wamiliki wa Hoteli ya kitalii ya Golden Tulip iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam wamekubaliana na uamuzi wa Serikali wa kukifuta rasmi Kiwanja namba 2048 ambacho awali walikimiliki.

Wamiliki hao walifika Ofisini kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Willium Lukuvi kueleza lengo lao la kuunga mkono mpango huo wa Serikali na kwamba wamekubaliana na uamuzi wa matumizi ya eneo hilo lililo karibu jirani na hoteli yao.

Wamesema wao ni raia halali wa Tanzania wanaoishi kwa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi na kamwe hawawezi kuingia kwenye mvutano na Serikali au kutotii maagizo yake.


Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwashukuru wamiliki hao kwa kukubaliana na uamuzi wa Serikali na akaongeza kwamba tayari Serikali imefuta rasmi hati iliyotolewa kwao juu ya umiliki wa kiwanja.

Awali, tarehe 30, Januari 2016 Serikali ililazimika kuvunja uzio wa eneo la kiwanja hicho namba 2048 Msasani Penisula kilicho jirani na hoteli ya Golden Tulip ili kuzuia uendelezaji wake kwa kuwa eneo hilo ni kwa ajili ya matumizi ya umma.

Umiliki wa kiwanja hicho ulibatilishwa rasmi tarehe 1, Februari 2016 na kurudishwa Serikalini baada ya kuonekana ulimilikishwa kinyume cha taratibu za Sheria za Ardhi.




No comments:

Post a Comment