Na MAELEZO
Chama Cha National Reconstruction Alliance (NRA) kutoka
Zanzibar kimethibitisha kushiriki uchaguzi wa marudio wa Zanzibar
unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu baada ya kikao kilichofanyika
Februari 15.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Tanzania Bara Hassan
Almasi Kisabya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam ambapo amesema kuwa Chama hicho kitashiriki uchaguzi wa marudio na kusisitiza
kuwa tamko lililotolewa na mgombea wao la kutoshiriki uchaguzi wa marudio
lipuuzwe kwani ni tamko lake binafsi na sio msimamo wa chama.
“Tamko lililotolewa tarehe 14/02/2016 Si Tamko la chama cha
NRA bali ni tamko binafsi na wale waliomuagiza kwani yeye hana mamlaka ya
kukisemea chama wala wagombea wengine wa chama pasipo Baraka na vikao halali
vya chama” alisema Kisabya.
Amesisitiza kuwa maamuzi ya chama ni sharti yatoke
katika chama na sio kwa mgombea na ikiwa yeye amejitoa anatakiwa afuate taratibu
za kisheria katika kujitoa kama alivyofuata sheria katika kugombea nafasi hiyo.
Aidha, Chama kinatoa taarifa kwa wagombea wote Zanzibar
kujiandaa na wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio
utakaofanyika Machi 20, mwaka huu ili kutimiza haki yao kikatiba na kuchagua
viongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo
Chama cha NRA ni miongoni mwa vyama 14 vilivyosimamisha
wagombea katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana katika Uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar uliofutwa kwa nafasi ya Rais.
No comments:
Post a Comment