Friday, February 12, 2016

NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO ATOA PONGEZI KWA TWIGA STARS



Na: Shamimu Nyaki - Maelezo

Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura ameipongeza timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Twiga Stars) kwa kufanya vizuri katika michezo mbalimbali wanayoshiriki ndani na nje ya nchi iliyopelekea kushika nafasi ya nane katika bara la Afrika kwa mwaka 2015.

Pongezi hizo amezitoa leo jijjini Dar es Salaam wakati alipozungumza na wachezaji hao katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) ambapo wameweka kambi kwa ajili ya kujianda na Mchezo wao dhidi ya Zimbabwe utakaochezwa mwezi wa tano mwaka huu.

Mhe. Wambura amewataka wachezaji hao kujituma kwa bidii, kuwa na nidhamu pamoja na kuzingatia maadili ya nchi yetu kwa kuwa wao ni mwanga wa jamii ili waweze kufika mbali kama mchezaji Mbwana Samatta.
“Mnapokuwa kambini zingatieni maadili, kanuni, sheria zilizopo na kuamini michezo ni ajira kwenu na inaweza kubadili maisha yenu kwa kujiunga katika vikundi mbalimbali vya uwezeshaji” Alisema Mhe. Wambura.

Aidha Katibu Mkuu wa Shrikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Bw. Mwesigwa Celestine akitoa taarifa fupi ya utendaji wa Shirikisho hilo amesema kuwa kwa upande wa wanawake TFF inafanya juhudi za kuanzisha ligi ya Taifa ya mpira wa Wanawake kutoa mafunzo kwa makocha wa mpira wa wanawake pamoja na kufuatilia vipaji vya watoto wa kike waliopo mashuleni.

Bw. Celestine ameeleza changamoto mbalimbali zilizopo ndani ya shirikisho hilo ikiwemo baadhi ya sheria na kanuni zinazosimamia masuala ya mpira wa miguu Tanzania na FIFA zimekuwa zikitofautiana na sheria za nchi kwa kuwa hazijafanyiwa marekebisho ili ziweze kua na uwiano ambapo Mhe. Naibu Waziri ameahidi kuzishughulikia.

Kwa upande wake kapteni wa Timu ya Taifa ya wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars) Bibi. Sophia Mwasikile amemshukuru Naibu Waziri kwa pongezi alizowapa na kuahidi kuwa wataendelea kufanya vizuri zaidi na kuitangaza nchi vizuri kupitia mchezo huo na kushika nafasi ya juu zaidi ndani na nje ya Afrika.

Timu ya mpira wa miguu ya Wanawake Twiga Stars imekuwa ni timu pekee Tanzania inayofanya vizuri katika michuano inayoshiriki japokuwa haina wadhamini hivyo ni wakati wa wadhamini kujitokeza kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri zaidi.

















No comments:

Post a Comment