WADHAMINI Wakuu wa timu ya Yanga Bia ya Kilimanjaro, jana wameikabidhi timu hiyo hundi ya sh.milioni 25 kama zawadi kwa timu hiyo kutwaa ubingwa msimu wa 2013/2014.
Akikabidhi hundi hiyo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema wamefurahishwa sana na ushindi wa Yanga na kwamba wamejidhatiti kusaidia timu ambayo imechukua ubingwa katika ligi yenye ushindani mkubwa kutokana na kuibuka kwa timu mpya zenye nguvu.
"Yanga imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa ligi kuu, na sio ajabu wao kuibuka na ubingwa katika ligi hiyo.Napenda kuwapongeza wachezaji wa Yanga, makocha na uongozi mzima wa timu hiyo kwa matokeo mazuri ya kushinda ligi kuu kwa mara ya 24 sasa," alisema Kavishe.
Alisema zawadi hiyo ni sehemu ya sh.bilioni 1.5 ya udhamini wa Kilimanjaro kwa Yanga na imetolewa kwa lengo la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa ushindi na kusaidia klabu katika maandalizi yake ya kimataifa ambayo tayari Yanga inasifa ya kushiriki kutokana na ubingwa huo.
Akipokea hundi hiyo Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema wanawashukuru sana bia ya kilimanjaro kwa mchango wao, kwani timu yao ni nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi bora pamoja na udhamini mkubwa wa bia hiyo.
"Mafanikio yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na bia ya Kilimanjaro, imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa timu msukumo uliopelekea mafanikio haya," alisema Mwalusako.
Alisema Yanga sasa ina nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa la kimataifa kutokana na mafanikio hayo, hivyo wanaamini kutokana na udhamini wa bia hiyo wataendelea kukua na kufanikiwa.
No comments:
Post a Comment