Thursday, May 16, 2013

BARTHEZ, CHANONGO WAITWA STARS


KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen jana ametaja kikosi cha wachezaji 26 watakaoingia kambini kujiwinda kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech, Morocco.

Katika kikosi hicho, Kim ameita wachezaji wapya sita ingawa baadhi yao wamewahi kuchezea timu hiyo, huku akiacha wengine watatu aliokuwa nao kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Morocco ambapo Taifa Stars ilishinda mabao 3-1.


Akiwataja wachezaji Wapya aliowaita katika kikosi hicho kitakachoingia kambini Mei 20, mwaka huu, kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ni Ally Mustafa, Vicent Barnabas, Juma Luzio, Haruna Chanongo, Mudhathiri Yahya na Zahoro Pazi.

Alisema katika kikosi hicho ameacha wachezaji watatau Shabani Nditi, Nassoro Masoud 'Cholo' na Issa Rashid.

Kocha huyo alitaja kikosi kizima kuwa ni Makipa ni nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na Salum Abubakar (Azam).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).

Kocha Kim alisema kikosi kitakachoingia kambini kitakuwa na wachezaji 24 ambapo Samata na Ulimwengu watajiunga na timu jijini Marrakech, lakini wachezaji atakaondoka nao Dar es Salaam kwenda Addis Ababa ni 22 ambapo ataacha kipa mmoja na mchezaji mmoja wa ndani.

Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.

Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.

Kim alisema kabla ya kwenda Morocco kikosi hicho kitapita jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya kirafiki Juni 2, mwaka huu dhidi ya Sudan.



No comments:

Post a Comment