Thursday, March 06, 2014

HATARI: ACHINJA MTOTO, AJISALIMISHA POLISI, MTOTO APONEA KIFO


Shinyanga

Mtoto mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa la tatu katika shule ya msingi Majengo wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, Said Joshua amenusurika kifo baada ya baba yake mzazi kujaribu kumchinja kwa madai ya kuchoshwa na gharama za kumtibu maradhi yanayomsumbua.

Tukio hilo limetokea juzi saa 11 alfajiri huko katika kijiji cha Majengo wilayani Kahama ambapo mkazi wa kijiji hicho aliyetajwa kwa jina la Joshua Salvatory (37) ambaye ni fundi baiskeli alimkamata mwanae huyo na kumchinja kwa kisu shingoni kwa lengo la kutaka kumuua.

Hata hivyo mashuhuda wa tukio hilo walisema kusudio la Joshua halikuweza kufanikiwa mbali ya kujeruhi vibaya koromeo la mtoto huyo ambaye aliokotwa akiwa ametupwa baada ya baba yake kubaini ameishakufa na yeye mwenyewe kukimbilia polisi kujisalimisha.

ENDELEA KUSOMA. . .

Mganga mfawidhi wa hospitali ya serikali wilayani Kahama, Dkt. Joseph Fwoma alithibitisha kufikishwa kwa mtoto huyo katika hospitali hiyo na wasamaria wema waliomuokota huku akiwa anavuja damu nyingi shingoni kutokana na jaribio hilo la kuchinjwa.

Dkt. Fwoma alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo madaktari walimfanyia upasuaji wa haraka na kumshona sehemu yote ya koromeo lililokuwa limechinjwa ambapo aliongezwa damu na kwamba hali yake kwa hivi sasa inaendelea vizuri.

Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto huyo ambaye waliishatengana na mumewe kwa kipindi kirefu, Mariamu Iddi (35) alisema alishitushwa na taarifa za kuchinjwa kwa mwanae ambaye alikuwa akiishi naye kwa kipindi kirefu kabla ya kuchukuliwa na baba yake siku moja kabla ya tukio hilo.

“Leo asubuhi (jana) nimepigiwa simu na kuelezwa taarifa za kuchinjwa kwa mwanangu, nilishituka sana, sikuamini kwamba juzi alimchukua kwa ajili ya kwenda kumuua, mara nyingi huwa akimchukua kwa lengo la kumtafutia matibabu kutokana na maradhi yanayomsumbua,”

“Lakini kila alipokuwa akimchukua alikuwa akimrudisha, katika siku za hivi karibuni alikuwa akilalamika mara kwa mara akidai amechoshwa na gharama za kumtibu kila mtoto mtoto, maana muda mrefu amekuwa ana tatizo la kiafya (hata hivyo ugonjwa haukatajwa), nahisi ni chanzo cha kutaka kumuua,” alieleza Mariamu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo hata hivyo alisema inahisiwa Joshua huenda anasumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa akili na kwamba baada ya uchunguzi wa kina atafikishwa mahakamani kujibu shitaka la kujaribu kuua.

Katika tukio lingine mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi sita ambaye hakufahamika jina wala makazi yake ameokotwa kichakani akiwa amekufa huku mwili wake ukiwa hauna jeraha lolote na ukiwa umeanza kuharibika.

Kamanda Mangalla alisema mwili huo uliokotwa na wapita njia juzi saa 12 jioni huko katika kijiji na Kata ya Mhongolo wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga ambapo ilionesha mtoto huyo alitupwa siku tatu zilizopita.

Hata hivyo alisema mpaka sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na polisi inaendelea na uchunguzi wa kina ili kuweza kumbaini na kumkamata mtu aliyefanya kitendo hicho ili aweze kufikishwa mahakamani.


No comments:

Post a Comment