Thursday, March 06, 2014

KENYA NAO WAANZA KULILIA SHERIA KALI DHIDI YA USHOGA

Mbunge Irungu Kang’ata anaongoza juhudi za kundi lililoundwa majuzi la kupinga wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya. Sheria zilizopo zasema ni hatia kwa watu kujiingiza katika tabia za ushoga na adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela.

Kenya huenda ikawa nchi inayofuata kwenye utata unaohusiana na haki za wapenzi wa jinsia moja, huku wabunge wakipanga kuwasilisha mswada bungeni kushinikiza serikali kufanya juhudi zaidi kutekeleza sheria zilizomo za kupiga marufuku ushoga.

Nao wanaharakati wa kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja wanasema shinikizo limeongezeka tangu nchi jirani ya Uganda kupitisha sheria dhidi ya mashoga mwezi jana.

Irungu Kang’ata, ambaye ni mbunge kwa mara ya kwanza anaongoza juhudi za kundi lililoundwa majuzi la kupinga wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya. Katika kampeni wazi kabisa mbunge huyo ameomba chama tawala kuelezea serikali inachukua hatua gani kutekeleza sheria zilizopo dhidi ya mashoga.

Sheria zilizopo nchini Kenya zinasema ni hatia kwa watu kujiingiza katika tabia za ushoga na adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela. Hakuna aliyewahi kushtakiwa nchini humo, lakini wanaharakati wanasema kuna kesi takriban 8 mahakamani ambazo hazijaamuliwa.

Kundi hilo linalopinga wapenzi wa jinsia moja liliundwa majuzi wakati rais wa nchi jirani ya Uganda Yoweri Museveni alipotia saini sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja mwezi Februari, licha ya shinikizo kutoka kwa nchi za Magharibi asitie saini.Sasa ushoga huko Uganda ni kosa linaloweza kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha jela.

Mbunge Kang’ata anasema anataka kuwasilisha mswada mpya utakaokuwa na adhabu kali zaidi nchini Kenya ikiwa bunge litaamua kuwa sheria zilizopo hivi sasa hazitoshi. Na anawashauri mashoga wajiepushe na matatizo haya kwa ‘kufyata midomo’.

Lakini kwa mkurugenzi wa kundi la kitaifa la tume ya haki za mashoga Kenya, Eric Gitari anasema shinikizo hili dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ni njia moja ya kugubika matatizo ya kisiasa yaliyomo na ukiukwaji wa haki za kibinafsi.

Gitari ambaye ni wakili wa kutetea haki za binadamu, anapinga pendekezo kwamba wapenzi wa jinsia moja wakae kimya, akisisitiza kuwa ni wanasiasa wanaolieneza swala hili kwa umma. Kama mwanamume ambaye ni shoga anasema mara nyingi anajihisi kama raia wa daraja la pili.

Naye mwanaharakati wa kibinafsi Kenne Mwikya, anasema hisia nchini Kenya zinaweka mazingira yafaayo kwa watu kama mbunge Irungu Kang’ata kuamua kuwa wanapaswa kubuni sheria mpya dhidi ya wapenzi wa jinsia moja au kutekeleza sheria zizilizopo.

No comments:

Post a Comment