Monday, April 16, 2018

MNEC: WAZAZI, UHURU KWA WATOTO UWE NA MIPAKA


PICHANI: Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Salim (RATCO) Mkoa wa Tanga, akizungumza kwenye Kongamano la Maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho na kufanyika Aprili 15, 2018 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).


Na Yusuph Mussa, Korogwe
Immamatukio Blog

MJUMBE wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Mohamed Salim (RATCO) amewaasa wazazi kuacha kuwapa watoto wao uhuru usio na mipaka, kwani kuendelea kuwaruhusu watoto kufanya wanavyotaka, ni kuongeza mmomonyoko wa maadili.

Aliyasema hayo juzi (Aprili 15) kwenye Kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho Wilaya ya Korogwe Mjini na kufanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, ambapo Salim alikuwa mgeni rasmi.

Salim alisema sio kwamba watoto hawana maadili, bali wanaangalia na malezi wanayolelewa na wazazi wao, hivyo wanapoona hawakemewi ama kuulizwa jambo lolote, hata kama wamefanya kitu kibaya, ndipo wanapoona wamepata njia ya mkato kutaka wafanyavyo.

"Wazazi tuna jukumu kubwa la kuwalea watoto wetu. Ni kweli tunawapenda na tumewapa uhuru wa kufanya mambo wanayoyataka, lakini uhuru huo uwe na mipaka na kuweza kuzingatia maadili yetu. Mtoto ni lazima awe mtiifu kwa wazazi wake, na akielezwa hili ni baya, basi aachane nalo" alisema Salim.

Salim, pia alizungumzia Shule za Sekondari za Jumuiya ya Wazazi ya CCM. Alisema shule hizo ambazo nyingi ni kongwe, ziweze kuboreshwa ili kuingia kwenye ushindani, kwani zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa walimu, vitendea kazi na uchakavu wa miundombinu ikiwemo madarasa, nyumba za walimu na mabweni.

"Lazima shule zetu tuziboreshe ili ziweze kushindana hasa kwenye kufaulisha watoto wetu. Lakini pia ziweze kuboreshwa miundombinu, vitabu na walimu" alisema Salim.

Salimu ambaye ni mmiliki wa mabasi ya Kampuni ya RATCO, alisema Serikali ni lazima itengeneze ajira kwa vijana ama sivyo vitendo vya uhalifu vitaongezeka, kwani vijana wengine wanashinda vijiweni, huwezi jua kwenye vijiwe vile wanapanga nini ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Korogwe Mjini Mohamed Mbuluazi alisema baada ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dkt. John Magufuli kuzungumzia mmomonyoko wa maadili kwenye Mkutano Mkuu wa Tisa wa Jumuiya ya Wazazi Taifa hivi karibuni mkoani Dodoma, wao kama jumuiya, waliamua kufanya kongamano hilo ili kuwa na mjadala mpana wa maadili.

Mbuluazi alisema Jumuiya ya Wazazi ya CCM ndiye yenye dhamana kuona inamuunga mkono Rais Dkt. Magufuli katika kurudisha maadili kwa watoto wetu, hasa ukichukulia jumuiya hiyo inamiliki shule, ambapo ndani ya shule hizo lazima wajenge nidhamu, maadili na unyenyekevu.

Alisema kama jumuiya, ni lazima wadumishe umoja, mshikamano, upendo na uadilifu ili jumuiya zote za CCM ikiwemo ya Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT) kuweza kukisaidia chama kupata ufanisi.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chifu Kimweri (Serikali) na Shule ya Sekondari Shemsanga (Jumuiya ya Wazazi CCM) wakishiriki Kongamano la Maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Korogwe Mjini mkoani Tanga, ambalo limefanyika juzi (Aprili 15) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio blog).


No comments:

Post a Comment