Monday, April 16, 2018

MJI WA KOROGWE NA JITIHADA ZA KUPATA MANISPAA

 Wakuu wa Idara wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambao walitembelea Stendi ya Mabasi Korogwe na Soko la Kimataifa kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe. Nia ya ziara hiyo ni kujifunza, kwani Manispaa ya Moshi inataka kujenga Stendi mpya ya Mabasi eneo la Majengo. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Na Yusuph Mussa, Korogwe
Immamatukio Blog

HALMASHAURI ya Mji Korogwe mkoani Tanga huenda ikapata hadhi ya kuwa Manispaa ama Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Usambara kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa inayojengwa kwenye mji huo. Hayo yamesemwa jana (Aprili 16) na watendaji na wataalamu wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, mara baada ya kutembelea miradi miwili ya Stendi Kuu ya Mabasi na Soko la Kimataifa mjini Korogwe.

Kiongozi wa Wakuu wa Idara na Vitengo wa Manispaa hiyo Danford Kamenya alisema wametoka Moshi kwenda kujifunza Korogwe baada ya kupata sifa kutoka Stendi ya Mabasi Korogwe kwa watu mbalimbali ikiwemo Rais Dkt. John Magufuli wakati anaifungua Agosti 7, 2017.

Kamenya alisema miradi hiyo miwili itaongeza mapato ya halmashauri hiyo pamoja na kuufanya Mji wa Korogwe kuwa na mvuto, hivyo kuweza kuingia kwenye hadhi ya Manispaa. "Tumekuja Korogwe kujifunza kwa vile na sisi Moshi tunajenga Stendi Kuu ya Mabasi eneo la Majengo. Lakini kwa mambo tuliyoyakuta Korogwe ni kiashiria tosha kwa halmashauri hii itapaa kimapato.

"Kwa kweli Halmashauri ya Mji wa Korogwe imeweza kujitengenezea vyanzo vya mapato ambavyo vitaweza kuwainua kutoka Halmashauri kwenda Manispaa" alisema Kamenya ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira ya Manispaa ya Moshi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri alisema Mji wa Korogwe una hadhi sio tu kuwa Manispaa, bali hata Makao Makuu ya Mkoa, kwani wana taasisi nyingi ikiwemo shule za sekondari zaidi ya nane, ambapo kati ya hizo, Shule ya Sekondari Joel Bendera, Semkiwa na Kwamndolwa zitakuwa na mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume, na baadhi ya mabweni yamekamilika.

Shauri alisema Halmashauri ya Mji Korogwe ina vyuo vya uuguzi viwili, hospitali mbili, vituo vya afya zaidi ya viwili na zahanati zaidi ya nne. Kuna vyuo vya ualimu viwili, utalii na shule za msingi na zile za mchepuo wa kingereza tatu, hivyo wapo kamili kuikaribisha Manispaa ama Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Usambara.

Kwa uchunguzi wa mwandishi, Halmashauri ya Mji Korogwe, ndiyo ya kwanza nchini kupata hadhi ya Halmashauri ya Mji nje ya makao makuu ya mkoa mwaka 2004. Halmashauri nyingine 11 zilizopewa hadhi mwaka huo ni pamoja na Kibaha (Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani) na Babati (Makao Makuu ya Mkoa wa Manyara).

Mkoa wa Tanga ni mkubwa ukiwa na Wilaya nane na halmashauri 11. Halmashauri saba zipo kwenye Wilaya za Lushoto, Korogwe, Handeni na Kilindi (Ukanda wa Usambara, huku Halmashauri nne zikiwa kwenye Wilaya ya Tanga, Muheza, Mkinga na Pangani (Ukanda wa Pwani).

Kilio cha wananchi wa Ukanda wa Usambara tangu Utawala wa Awamu ya Nne, ni kuomba Mkoa wa Tanga kugawanywa ili kusogeza karibu maendeleo ya wananchi, kwani Mkoa wa Katavi wenye watu 564,604 kwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi hiyo ni sawa na wananchi wa Wilaya ya Lushoto yenye halmashauri mbili, Bumbuli na Lushoto, kwani ina watu 492,441 (mwaka 2012).

No comments:

Post a Comment