Thursday, March 08, 2018

MBUNGE AMUOMBA MKURUGENZI KOROGWE MJI KUWAOKOA WANAFUNZI

Madarasa haya ndiyo yanatumika kwa sasa Shule ya Msingi Msambiazi, Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe. Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda ambaye amefika shuleni hapo leo Machi 8, 2018, kukagua ujenzi wa madarasa mapya matatu na ofisi mbili za walimu kwenye shule hiyo, ameitaka Halmashauri ya Mji Korogwe kutafuta fedha kumalizia ujenzi wa madarasa hayo ili kuwaondolea adha wanafunzi wanaosoma kwenye madarasa haya, ambayo mabati yake pia yanavuja ikinyesha mvua.(Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog)
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda leo Machi 8, 2018 amefika Shule ya Msingi Msambiazi, Kata ya Mtonga katika Halmashauri ya Mji Korogwe ili kukagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi mbili za walimu. Pichani Chatanda akiangalia choo kipya kwenye shule hiyo, ambapo ili kukamilisha ujenzi wa choo hicho, ametoa sh. milioni 1.5 kupitia Mfuko wa Jimbo.(Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog)

Na Yusuph Mussa, Korogwe
IMMAMATUKIO BLOG

MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri, kutafuta fedha haraka ili kukamilisha ujenzi wa madarasa matatu na ofisi mbili za walimu Shule ya Msingi Msambiazi.

Ni baada ya kufanya ziara kwenye shule hiyo leo Machi 8, 2018 na kukuta baadhi ya madarasa ya shule hiyo ni tishio kwa usalama wa wanafunzi, kwani kuta na madirisha vinataka kuanguka, hivyo kufungwa kamba ili kuzuia mabati yasiezuliwe na upepo, huku mabati hayo yakiwa yametoboka.

Chatanda alisema wasisubiri watoto hao kupata madhara, bali wachukue hatua kwa kumaliza ujenzi wa maboma hayo ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi, Serikali na wahisani.

"Ofisa Ellimu Msingi (Elias Mavoa) naomba umfikishie salamu Mkurugenzi wa Halmashauri (Shauri). Atafute fedha za haraka tumalize madarasa haya, kwani madarasa haya ya sasa ni machakavu na mimi mwenyewe nimeyaona... haiwezekani dirisha na mbao za bati ziwe zimeshikiliwa na kamba.

"Lakini kama alivyosema Mwalimu Mkuu (Zena Machite) wakati anatoa taarifa yake, ndani ya madarasa hayo mvua ikinyesha kunavuja na inabidi kuhamisha wanafunzi kwenye madarasa hayo wakati wa mvua" alisema Chatanda.

Mkuu wa Shule Machite, alisema moja ya changamoto kwenye shule hiyo ni uchakavu wa madarasa matatu na ofisi mbili, ile ya Mwalimu Mkuu na Ofisi ya Walimu.

Machite alisema mpaka sasa ujenzi wa madarasa hayo matatu na ofisi mbili za walimu umegharimu sh 12,898,000 na hadi kukamilika utagharimu sh. milioni 44.1. Na baadhi ya wadau waliochangia ni jamii sh. milioni 1.9, Mfuko wa Jimbo sh. 575,000, harambee ya wadau wengine sh. 423,000 na fedha kutoka halmashauri sh. milioni 10.

Machite alisema wanajenga choo kipya chenye matundu 10 kutokana na choo kilichopo kuwa chakavu na kuhatarisha afya na usalama wa wanafunzi, kwani wakati wowote kinaweza kuanguka.

Alisema hadi sasa ujenzi umebakia umaliziaji ambapo ni milango na madirisha ya vyoo na rangi kwenye baadhi ya maeneo, ambapo hadi sasa ujenzi wa choo hicho umetumia sh. milioni 9.8, na ili kukamilisha kunahitajika sh. milioni 1.5.

Hata hivyo Chatanda ameahidi kumalizia ujenzi wa choo hicho kwa kutoa sh. milioni 1.5 kupitia Mfuko wa Jimbo, huku Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Mavoa akimshukuru Chatanda kwa kutoa sh. milioni 1.5 kumalizia ujenzi wa choo.



Madarasa matatu na ofisi mbili za walimu Shule ya Msingi Msambiazi, Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe. Hadi sasa ujenzi huo umegharimu sh. milioni 12 na hadi kukamilika itakuwa sh. milioni 44.(Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog)
Choo kinachotumika sasa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Msambiazi, Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe, ambapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Zena Machita alimueleza Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda kuwa choo hicho sio salama tena kwa matumizi kutokana na uchakavu wake.(Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog)

Dirisha likiwa limefungwa kamba ili kuzuia paa la bati lisije likaezuliwa na upepo kwenye Shule ya Msingi Msambiazi, Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe. Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda (pichani) alibaini uchakavu huo baada ya leo Machi 8, 2018 kufika hapo ili kukagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi mbili za walimu. Ameitaka Halmashauri ya Mji Korogwe kuharakisha kumaliza majengo hayo ili kuwanusuru wanafunzi kuangukiwa na kuta za madarasa.(Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog)
 (Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog)


No comments:

Post a Comment