Tuesday, December 19, 2017

TANESCO YAJIVUNIA UMEME WA UHAKIKA PANGANI HYDRO



Na Mwandishi Wetu, Korogwe

SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO), litaendelea kuzalisha umeme wa uhakika katika vituo vyake vitatu vya Pangani Hydro Systems ambavyo kwa sasa vinazalisha megawati 97.

Vituo hivyo ni Hale kilichopo Wilaya ya Korogwe, New Pangani Falls, Wilaya ya Muheza, vyote vipo Mkoa wa Tanga na Nyumba ya Mungu kilichopo katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Meneja wa vituo hivyo Mhandisi Mahenda Mahenda(Pichani Juu), aliyasema hayo Mjini Korogwe jana wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini. Wahariri hao wapo katika ziara ya kutembelea vituo vya uzalishaji umeme, kungalia changamoto na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya umeme nchini.

Mhandisi Mahenda alisema, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika vituo hivyo ikishirikiana na wafadhili ili kujihakikishia upatikanaji umeme wa uhakika, kuchochea maendeleo ya jamii na kuvutia uwekezaji, ujenzi wa viwanda nchini.

Alisema ili kuunga mkono juhudi za Serikali, vituo hivyo vina msaada mkubwa wa kuzalisha umeme amboa huingizwa katika gridi ya Taifa mbali ya uwepo wa changamoto ya ubovu wa mtambo mmoja katika kituo cha Hale.

"Uwezo wa Kituo cha Hale ni kuzalisha megawati 21, kwa sasa kinazalisha megawati 8 kutokana na mtambo mmoja kuharibika tangu mwaka 2004 "Hivi sasa tupo katika mchakato wa kufanya ukarabati mkubwa katika kituo hiki sambamba na kubadilisha mitambo ya uzalishaji umeme ambayo ilianza kufanya kazi mwaka 1964," alisema.

Aliongeza kuwa, ukarabati huo pia utahusisha miundombinu yote ambayo ni shirikishi ambapo vituo vya New Pangani Falls, Nyumba ya Mungu navyo vitafanyiwa ukarabati kulingana na hitaji la matengenezo yanayohitajika kwa sasa.

Mhandisi Mahenda alisema New Pangani Falls kinazalisha megawati 68 na Nyumba ya Mungu megawati 8 ambapo baada ya ukarabati wa Kituo cha Hale kukamilika, uzalishaji utaongezeka.

"Kuna mpango madhubuti wa kufanya ukarabati wa mitambo katika vituo vyote vitatu kwa kutumia Wakandarasi wakubwa wenye nyenzo za kisasa na utaalamu mkubwa.

Ukarabati kwenye Kituo cha Hale utahusisha uwekaji wa mifumo, kubadili jenereta, kuboresha njia za kuingiza, kutoa watu na mizigo mgodini, kujenga upya kituo cha kupozea umeme," alisema.

Mradi katika kituo hicho ulianza mwaka 2016 baada ya kukamilika kwa mchakato wa kumpata Mkandarasi Mshauri kampuni kutoka Sweden inayoitwa Sweco International ikishirikiana na Energy Infratech Private Ltd ya India.

Utekelezwaji wa mradi huo utaanza muda wowote baada ya Mkandarasi ambaye atashinda zabuni ya matengenezo kwa miezi 31 ambapo wakati wa matengenezo uzalishaji umeme utaendelea.



Akizungumzia changamoto, alisema ni pamoja na kupungua maji ya kuzalisha umeme kutokana na kuharibika kwa kingo za mito inayoingiza maji Bwawa la Nyumba ya Mungu.



Changamoto nyingine ni kuharibika kwa kingo za Mto Pangani zinazopokea maji kutoka Nyumba ya Mungu hadi kituo cha Hale hali inayokufanya kituo cha Nyumba ya Mungu kizalishe megawati 3.5 badala ya 8.



Nyingine ni ongezeko la matumizi ya maji katika shughuli za kilimo, wakulima kulima hadi kwenye kingo za mto na umri mkubwa wa mitambo ya kuzalisha umeme katika kituo cha Hale.

No comments:

Post a Comment