Wednesday, December 20, 2017

MITO YA ASILI YACHANGIA UPOTEVU MAJI NYUMBA YA MUNGU




Na Mwandishi Wetu, Mwanga

ONGEZEKO la shughuli za kilimo kupitia mito ya asili isiyosakafiwa pembezoni mwa Bwawa la Nyumba ya Mungu linachangia upotevu mkubwa wa maji, kupunguza uzalishaji wa umeme katika vituo vya Pangani Hydro Systems.

Vituo hivyo ni Nyumba ya Mungu, kilichopo Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, New Pangani Falls, Wilaya ya Muheza na Hale kilichopo Wilaya Korogwe, mkoani Tanga.

Meneja wa vituo hivyo Mhandisi Mahenda Mahenda, akiyasema hayo jana wakati akielezea umuhinu wa Bwawa hilo kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini. Wahariri hao wapo katika ziara ya kutembelea vituo vyote vya kufua umeme kwa njia ya maji ili kujionea uzalishaji, chanamoto zilizopo.

Alisema Nyumba ya Mungu kuna mitambo miwili inayozalisha umeme wa megawati 8 iliyoanza kazi mwaka 1969, mitambo hiyo iko vizuri na imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara. "Bwawa linapokuwa na kiwango kidogo cha maji uzalishaji umeme hupungua, kuna wakati maji hupungua zaidi hivyo taratibu haziruhusu tuendeleekuzisha umeme.

"Ili tuendelee kuzalisha, tunapaswa kupata kibali kutoka Wizara ya Maji ambao ndio wamiliki wa bwawa hili," alisema Mhandisi Mahenda. Aliongeza kuwa, bwawa hilo ni chanzo kikubwa cha uzalishaji umeme katika vituo hivyo ambavyo vyote vinazalisha megawati 97 ambao huingizwa kwenye gridi ya Taifa kwa matumizi mbalimbali  ya majumbani na viwandani.

Kwa upande wake, Fundi Sanifu Mkuu kutoka Bonde la Mto Pangani (PBWO), Vendelin Baso, alisema wanafanya jitihada kubwa ya kulinda mazingira ya Bwawa hilo ili yasiharibiwe. Amisema PBWO imekuwa ikishirikisha viongozi wa vijiji vilivyopakana na bwawa hilo ili wawe na matumizi bora ya maji ili kupunguza upotevu wa maji katika mito ya asili isiyosakafiwa.

Alisema bwawa hilo lilianza kutumika mwaka 1968 kwa lengo la kudhibiti mafuriko na kilimo cha umwagiliaji kwa wananchi.

"Naziomba Mamlaka zinazohusika ziwajibike kuhamasisha uboreshaji mifereji kwa kuisakafia ili kuokoa upotevu mkubwa wa maji, tuondokane na mifereji ya asili isiyosakafiwa ambayo inapoteza maji mengi ya bwawa hili," alisema Baso.


No comments:

Post a Comment