Thursday, October 12, 2017

TANESCO YALETA MATUMAINI MAPYA KATIKA HALMASHAURI YA MADABA


 Mhandisi Didas Lyamuya (katikati nyuma mwenye vesti ya kijani) akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa kitongoji cha Madaba pamoja na baadhi ya wahariri walioshiriki katika ziara ya kujionea miradi mbalimbali iliyowekezwa na TANESCO katika kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapata umeme. Kushoto aliyeinama ni Leilah Muhaji, Kaimu Afisa wa Uhusiano wa TANESCO, wengine ni Lilian Timuka kutoka Mwananchi, Mariam Mziwanda (kutoka kulia) na katikati aliyebeba mtoto ni Nevile Meena, Na Joyce Shebe, kushoto mwenye nguo nyekundu.



Na Mwandishi Wetu, Njombe


HALMASHAURI ya Mabada, mkoani Njombe, iko mbioni kuweka historia ya kuondokana na giza ifikapo Desemba, mwaka huu. Tangu uhuru na baada ya kuanzishwa halmashauri hiyo, haijawahi kuwa na umeme hali iliyochangia kukwamisha maendeleo ya wananchi kiuchumi.

Ili kukuza hadhi ya halmashauri na uchumi wa wananchi, Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO), limekamilisha uwekaji wa nguzo za umeme na utandikaji waya ili kuunganisha umeme kwa wananchi.

Kukamilika kwa kazi hiyo ni matokeo ya mradi mkubwa wa umeme wa kilovolti 220kV kutoka Makambako hadi Songea unaotekelezwa na Serikali uliogawanyika katika sehemu tatu. Meneja wa mradi huo, Mhandisi Didas Lyamuya, aliyasema hayo Mjini Madaba jana wakati akitoa ufafanuzi wa mradi kwa Wahariri wa vyombo vya habari waliopo katika ziara ya kuangalia maendeleo ya mradi huo.


Alisema mradi unahusisha mfumo wa usafirishaji njia za umeme msongo wa kilovolti 220/132/33kV kwa umbali wa kilomita 250 na ujenzi wa vituo vitatu vya kupoozea umeme.

Vituo hivyo vinajengwa Makambako, Madaba na Songea ambapo mradi umefadhiriwa na Serikali ya Tanzania, TANESCO na Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la maendeleo (SIDA). Alisema ujenzi wa vituo hivyo upo katika awamu mbalimbali ukitarajiwa kukamilika Machi,2018 na uwekaji nguzo za umeme wa kilovolti 220kV utakuwa umekamika ifikapo Januari,2018.

"TANESCO inatekeleza kwa vitendo agizo la kufikisha umeme katika Halmashauri ya Madaba ili kuchochea shughuli za kiuchumi. "Pia upatikanaji umeme Madaba utaharakisha maendeleo ya wananchi, halmashauri, kuongeza usalama maeneo ya wananchi, kuboresha huduma za afya na kufungua fursa ya ujenzi wa viwanda," alisema.

Aliongeza kuwa, kwa kuanzia Madaba itapata umeme ambao utazalishwa na jenereta ambazo zipo katika hatua ya kufungwa, ifikapo Desemba, mwaka huu, umeme utakuwa umewaka. Mhandisi Lyamuya alisema Madaba ni mji mkubwa wenye nyumba zaidi ya 1,000, ambapo wananchi waliokamilisha taratibu za kuunganishiwa umeme ni 700 wakitarajia kupata wateja wengi zaidi.

"Tumefunga transfoma sita, mahitaji ni transfoma saba ili kuharakisha upatikanaji umeme, baada ya kukamilika mradi wa Madaba, matumizi ya jenereta yatasitishwa," alifafanua. Katika hatua nyingine, Mhandisi Lyamuya alisema Msitu wa Hifadhi wa Wino, unaweza kuwafanya wakazi wa vijiji mbalimbali kutofikiwa na neema ya umeme unatokana na mradi huo.

Alisema uongozi wa msitu umegoma kuruhusu upitishaji nguzo ya 33kV ili uweze kuvifikia vijiji mbalimbali kikiwemo Kijiji cha Kifanya, kazi hiyo imeshindwa kufanyika kuanzia Mei, mwaka huu.

"Kuna tatizo la sera ya hifadhi, hawaruhusu kupitisha nguzo hadi walipwe fidia wakati kwa upande wetu, upitishaji nguzo za 33Kv, kisheria TANESCO hailipi fidia lakini mazungumzo bado yanaendelea ili waturuhusu," alisema.

Aliongeza kuwa, upitishaji nguzo katika eneo la hifadhi utakuwa na urefu wa kilomita tatu na upana wa mita 10 ili Kijiji cha Kifanya na vingine vinufaike na mradi huo. Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gabriel Lwesya, alisema mradi utazinufaisha Wilaya tano, halmashauri moja.

Wilaya hizo ni Songea Mjini, vijijini, Mbinga, Namtumbo, Nyasa na Halmashauri ya Madaba hivyo alitoa wito kwa wawekezaji kujitokeza kwa wingi ili kujenga viwanda. Alisema mradi huo utafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi ambao kuanzia mwanzoni mwa 2018 watapata umeme wa uhakika.

Akizungumzia jinsi wanavyoupokea mradi huo, mkazi wa Madaba, Upendo Michael, aliishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao kwani umeme wanaotarajia kupata, utabadili maisha yao. Aliongeza kuwa, wakazi wengi wa Madaba wanapenda kufanya shughuli za ujasiriamali lakini walishindwa kwa sababu hawana umeme.

"Kuja kwa umeme kutapunguza matukio ya uharifu, ubakaji na wizi yaliyoshamiri hasa katika maeneo yenye giza, baadhi ya wananchi wenye kipato wanatumia sola, majenereta," alisema.

Naye Meneja anayesimamia ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme 220/33kV cha Madaba, Waney Xiao, alisema kasi ya ujenzi ni nzuri, kukamilika kwa ujenzi huo kutainua maisha ya wananchi kiuchumi na kukuza kipato chao.

No comments:

Post a Comment