Friday, October 13, 2017

TANESCO: NJOONI MUANZISHE VIWANDA RUVUMA. WATEJA ZAIDI WAUNGANISHIWA UMEME

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

SHIRIKA la umeme nchini (TANESCO), limesema kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme kutoka Makambako, mkoani Njombe hadi Ruvuma ni fursa nzuri kwa wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba 2018 na kuzalisha umeme wa uhakika katika makazi ya watu na kwenye viwanda ambavyo vitatoa ajira kwa wananchi, wengine kujiajiri wenyewe.

Meneja wa mradi, Mhandisi Didas Lyamuya, aliyasema hayo Mjini Songea, mkoani Ruvuma jana wakati akielezea faida za mradi huo kwa Wahariri vya vyombo mbalimbali vya habari. Wahariri hao walitembelea kituo cha kupoozea umeme kunachojengwa mkoani humo 220/33kV ambacho ujenzi wake ukikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 60 za umeme.


Ujenzi wa kituo hicho na vingine viwili kimoja kikiwa Makambako na Madaba, mkoani Njombe, unafanywa na Serikali kupitia TANESCO. Mbali ya vituo hivyo, pia mradi huo unahusisha mfumo wa usafirishaji umeme wa 220kV kutoka Makambako hadi Songea, kujenga mfumo wa kusambaza umeme wa 33kV.

Akizungumza na Wahariri hao, Mhandisi Lyamuya alisema kituo hicho kitapokea umeme unaotoka Madaba ambacho nacho kitapokea nishati hiyo kutoka kituo cha Makambako. Mradi huo umefadhiriwa na Serikali ya Tanzania, TANESCO na Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la Maendeleo (SIDA).

"Katika kituo cha Songea, tutafunga transfoma mbili kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 30 hivyo zote mbili zitazalisha umeme wa megawati 60," alisema. Aliongeza kuwa, hivi sasa wakazi wa Songea wanapata umeme unaozalishwa na jenereta za TANESCO zinazotumia mafuta ya dizeli.

"Changamoto zilizopo kwenye mradi huu ni ongezeko la wateja, hivi sasa mahitaji ya umeme kwa Mkoa mzima ni Megawati 5.35. Kati ya umeme huo, megawati 4.8 wanazinunua kutoka kwa Watawa wa Tulila ambapo shirika hilo huzalisha megawati 1.5, wakati wa kiangazi, Tulila hupunguza hitaji la megawati hizo.

"Kituo cha Ruvuma kitalusha umeme kwenye Wilaya za Songea, Mbinga, Nyasa na Namtumbo, baada ya mradi kukamilika jenereta zilizopo Songea zitazimwa," alifafanua.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO mkoani humo, Mhandisi Patrick Lwesya, alisema gharama za kuendesha jenereta zinazozalisha umeme eneo la Lizabon ni kubwa hivyo kukamilika kwa mradi huo kutapunguza gharama za uzalishaji.

Alisema kituo cha kupoozea umeme 33/11 kV kilichopo Songea kitazalisha megawati 10 wakati mahitaji ya sasa mjini humo ni medawati 5.35. Mhandisi Lwesya alisema shirika hilo kwa sasa linatumia lita 12,000 za mafuta ya dizeli kila siku ili kuendesha jenereta hizo wakati shirika likiuza uniti moja ya umeme kwa sh. 560.

"Tunatarajia kupata wateja wengi wapya baada ya kukamilika kwa mradi maana tutakuwa na umeme mwingi wa uhakika, hadi Desemba, mwaka huu tutaunganidha umeme kwa wateja wapya 10,000. "Katika Kijiji cha Kigonsela, tumepata wateja wapya 200, kati yao 110 wamelipia," alisema.


No comments:

Post a Comment