Saturday, September 02, 2017

SHAKA AZUNGUMZIA MAENDELEO YA UCHAGUZI WA NDANI WA UVCCM

Ndugu Waandishi wa habari;

Kwa mara nyingine tena tunawakaribisha kwa mikono miwili katika mkutano huu muhimu. Karibuni sana huku nikiwaomba mjione mko huru na mko nyumbani .

Dhana ya Demokrasia ni jambo muhimu linalohitaji kuheshimiwa na kuenziwa ndani ya Chama na Jumuiya zake. Kiongozi wa UVCCM mahali popote pale huchaguliwa kwa kufanyika uchaguzi huru na wa haki unaozingatia Kanuni na Taratibu za Uchaguzi kama zilivyoagizwa na vikao husika bila ya kukiuka, kupuuzwa au kuvunjwa.

Nia ya UVCCM ni kujenga na kudumisha haiba njema ya kuendelea kuheshimu misingi ya demorasia ya kweli , yenye kuchunga adabu na kufuata nidhamu, miiko na maadili kwa kila mwanachama anayetaka kutumia haki ya kuchagua au kuchaguliwa.

April Mwaka 2017 Chama Cha Mapinduzi kilianza mchakato wa Uchaguzi ndani ya Chama na Jumuiya zake. Kufuatia mabadiliko ya Kanuni ya UVCCM yaliyofanyika mwezi Machi, 2017 tulianza Uchaguzi katika ngazi za Matawi ambapo hadi leo jumla ya Matawi 23,529 sawa na Asilimia 99.4% kati ya Matawi 23,670 sawa na Asilimia 0.59% yamekamilisha uchaguzi.


Ngazi za Kata 3,913 sawa na Asilimia 96.59% kati ya Kata 4,051 sawa na asilimia 3.4% zimekamilisha uchaguzi .Kwa upande wa majimbo ya Zanzibar majimbo 54 sawa na Asilimia 100%, wamekamilisha uchaguzi.

Ngazi ya Wilaya na Mkoa mchakato wa uchujaji wa majina kwa Vijana waliomba nafasi mbali mbali ndani ya Jumuiya yetu , umeanza na unaendelea vizuri huku jumla ya Vijana 7,606 wamejitokeza kuchuka fomu za kugombea nafasi mbali mbali katka Jumuiya yetu, hali inayoonyesha kumekupo kwa mabadiliko na msisimko wa kisiasa ukilinganisha na chaguzi zilizopita.

Kwa upande wa ngazi ya Taifa Vijana 350 wamejitokeza kuomba nafasi za uongozi ndani ya UVCCM kama ifuatavyo:-

(i) Nafasi ya Mwenyekiti 113 Walioomba
(ii) Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa 24 Walioomba
(iii) Nafasi 5 za Wajumbe wa H/Kuu 103 Walioomba
(iv) Nafasi 5 za Wajumbe wa B/Kuu Taifa 81 Walioomba
(v) Nafasi 1 Wawakilishi UWT 14 Walioomba
(vi) Nafasi 1 Wawakilishi Wazazi 15 Walioomba

Maandalizi kwa ajili ya Mikutano Mikuu ya Wilaya hadi Taifa yanaendelea vyema ambapo chaguzi zote ndani ya UVCCM zinategemewa kukamilika Novemba 2017.

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunaendelea kusisitiza kuwa sifa na wasifu wa kila mgombea aliyeomba kuteuliwa kwa kadri alivyojaza kwenye fomu yake, utaandaliwa na kuandikwa vizuri katika kitabu maalum cha wagombea wote ambacho watapatiwa wajumbe wa Mkutano siku ya uchaguzi husika.

Kila mgombea atapata nafasi ya kujieleza na kutoa wasifu wake, kutaja dhamira na malengo yake mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu husika baada ya taratibu za vikao vya uteuzi kukamilika si kinyume na hivyo.

Tunaendelea kuwakumbusha kuwa ni mwiko kwa mgombea kuanza kampeni mapema au wapambe wake kufanya ushabiki wa kisiasa kumnadi, kumpigia debe, au kujipitisha na kuelezea nafasi anayogombea. Ukiukaji huo wa Kanuni na taratibu utampotezea sifa za kuteuliwa.

Aidha tunaendelea kuwasisitiza kuwa ni marufuku na hairuhusiwi kabisa walioomba nafasi mbali mbali kuanza kufanya kampeni za kihuni , kutumia lugha chafu, siasa za maji taka kuchafuana, matusi, dharau kinyume na ubinadamu.

Kuyaacha hayo yote yafanyike bila ya kuyadhibiti, kuyaasa na kuyakemea ni mwanzo wa kukaribisha mvurugano, mgawanyiko hatimaye kujipenyeza kwa adui rushwa. Hivyo basi tunaendelea kuwaagiza watendaji wote wa ngazi husika kusimamia matakwa ya Kimaadili, Kikanuni na Kikatiba.

Aidha tunaendelea kuviomba vyombo vinavyohusika katika ngazi zote hasa TAKUKURU kuendelea na kufuatilia kwa karibu nyendo za wagombea na wapiga kura ili kubaini kuwadhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria. Mgombea au mpiga kura yoyote atakayethibitika kutoa au kupokea Rushwa, hatua za kimaadili na kisheria tunaelekeza zichukuliwe ili kulinda heshima ya taasisi yetu.

Tunaendelea kusisitiza kuwa uchaguzi wa UVCCM katika ngazi zilizobakia zitafanyika kwa misingi ile ile ya uhuru na uwazi huku kila mgombea akipitishwa na vikao vya kikanuni na kikatiba baada ya kukidhi mashariti ya uchaguzi kwa mujiba kanuni na katiba.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na malumbano yenye kupandikiza chuki na kupalilia mifarakano isio na ulazima huku baadhi wa watu wakiwachafua wenzao kwenye mitandao ya kijamii na wakati mwingine wapo wanaothubutu kuwatukana wenzao matusi ya nguoni kinyume na ustaarabu, ubinadamu na misingi na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi.

Wapo baadhi yao hujivika kofia ya Jumuiya wakitumia njia hatari na batili, wamekuwa wakikebehi, kutuhumu wenzao kinyume na utaratibu huku baadhi yao hata kufikia kutoa madai yanayovuka mipaka na kubeba taswira ya Jinai au madai.

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi umestushwa na hali hiyo inayoonekana kutaka kuibua migogoro na kujenga mazingira yanayotaka kuonyesha kana kwamba ndani ya Jumuiya kuna mvurugano au kuporomoka kwa mshikamano wetu wakati mambo nayo hayapo.

Kimsingi yote yanayofanyika ni kinyume na utamaduni wa Chama Cha Mapinduzi Kikatiba na Kikanuni na Kimaadili. CCM si genge la wahuni bali ni Chama makini cha Siasa kinacho heshimu utu wa mtu, taratibu na miongozo iliyojiwekea katika kushughulikia mambo yake.

Kwa miaka yote wanajumuiya na viongozi wamekuwa wakiishi kwa kuzingatia misingi ya Umoja, Upendo, mashauriano na kudumisha Maelewano.

Jumuiya yetu imekuwa ikifanya kazi zake kwa uwazi na umakini mkubwa. Tusingependa kuona ikitiwa nyufa au kukumbwa na athari za kutengenezwa na watu wachache. Nasema tena hatutasita kuchukua hatua stahili kwa mujibu wa kanuni Katiba ya Chama na ikibidi hata kisheria ili kukomesha vitendo hivyo vyenye nia ya kuondosha haiba nzuri ya Chama na Jumuiya katika kufanya mambo yake ya msingi.

Tumeanza kuwafatilia kwa karibu mno na kuanza kuwatambua wote ambao wanafanya au kushiriki vitendo hivyo vya aibu aidha iwe kwenye Jumuiya au ndani ya Chama chetu

Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake hujadili mambo yake aidha yakiwa magumu au mepesi kwa mujibu wa ajenda na njia za majadiliano kupitia vikao halali hatimaye maamuzi hutolewa baada ya kujiridhisha.

Kimsingi utaratibu wa kushughulikia mambo mbali mbali ndani ya chama na Jumuiya zake uko wazi.

Yeyote mwenye madai, tuhuma au shutuma anatakiwa atumie vikao halali vya kikanuni na kikatiba ama kuyafikisha kwa viongozi husika kwa kufuata utaratibu si kinyume na hivyo.

Kwa kila mwana jumuiya muadilifu, msemakweli, mpenda Umoja na Mshikamano, siku zote huheshimu kanuni, taratibu, katiba na maelekezo yanayotolewa na viongozi wetu.

Ndugu Waandishi wa habari.

Nachukua nafasi hii kuwaasa na kuwonya wale wote ambao pengine watakuwa wameteleza na kujikuta wakijielekeza katika kushiriki vitendo hivyo vyenye muoneekano wa uasi , tunawataka wajiepushe navyo hasa kipindi hiki ambacho tunaelekea katika Demokrasia ya kweli ndani ya Jumuiya.

Narejea tena wapo tunaowajua wakishiriki kufanya vitendo hivyo na kadri itakavyothibitika kwa kukusanya ushahidi na vielelezo , hatua za kikanuni, kikatiba na pale itakapobidi hatutasita kuchukua hatua za kisheria ili liwe funzo kwa wengine.

Tusingependa kuona watu wanajitwika na kubeba agenda binafsi au kufikiria kumchafua mtu ndio kupata cheo ndani ya Jumuiya yetu hakuna utamaduni huo haki na usawa itasimamiwa muda wote . Mtu yeyote atayendeleza kufanya hivyo kwa kisingizio cha Uchaguzi wa Chama na Jumuiya zake, mambo hayo hayakubaliki na hayatavumiliwa tena.

Ndugu waandishi Habari

Uchaguzi ni kipimo cha kupevuka na kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya kweli bila mizengwe au hila ndani ya chama na Jumuiya kwa lengo la kusimamia shabaha na misingi sahihi itokanayo na miongozo, maelekezo na kuheshimu utaratibu unaohimizwa na Chama Cha Mapinduzi .

Ili kuonyesha kutii na kufuata maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Mwenyekiti wetu wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli kila mwanachama anapaswa kujitambua, kujiheshimu, kufuata misingi ya katiba na kulinda kwa nguvu zake zote heshima ya Chama Cha Mapinduzi.

Ahsanteni sana na kila la heri.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Shaka Hamdu Shaka (MNEC)

KAIMU KATIBU MKUU




No comments:

Post a Comment