Thursday, May 18, 2017
TGNP YASEMA BAJETI YA ELIMU 2017/2018 HAIJATOA KIPAUMBELE KWA MTOTO WA KIKE
PICHA: Ofisa wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Veronica Magayane akitoa mada wakati wa mkutano wa uchambuzi wa bajeti ya wizara hiyo kwa mlengo wa kijinsia uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Na Dotto Mwaibale
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesema bajeti ya mwaka 2017/2018 ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iliyopitishwa na bunge haijatoa kipaumbele kwa mtoto wa kike.
Hayo yalibainishwa na Ofisa wa TGNP, Veronica Magayane wakati akitoa mada katika mkutano wa uchambuzi wa bajeti ya wizara hiyo kwa mlengo wa kijinsia uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alisema licha ya bajeti hiyo kupitishwa na bunge haijaangalia changamoto zinazomkabili mtoto wa kike kama umbali kutoka makazi na shule, kiwango cha walimu kisicholizisha, kutokuwepo kwa mabweni ya watoto wa kike, kufanyishwa kazi nyumbani kwa walimu kama kuchota maji na kuwapakia walimu.
Alitaja changamoto zingine ni kukosekana kwa maji ambapo kumechangia kuwafanya watoto hao wa kike kuwa katika wakati mgumu hasa wanapokuwa kwenye hedhi. "Changamoto hizi zote zimesababisha elimu kwa mtoto wa kike kushuka na kupelekea wengi wao kutofikia ndoto zao" alisema Magayane
Alisema matatizo mengi ya miundombinu ambayo huathiri zaidi watoto wa kike yanatokana na changamoto za mfumo wa bajeti ya sekta ya elimu hivyo suala la kuboresha miundombinu ya shule linapaswa kuwa kipaumbele zaidi kwa kuongeza fedha za bajeti ya maendeleo.
Akichangia katika mjadala huo, Mzee Hamisi Katumwa alisema kuna kila sababu ya kutenganisha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Elimu ili kupunguza kutupiana mpira ambapo kumekuwa na ucheleweshaji wa maamuzi ambapo mtu akienda Tamisemi anaambiwa suala hilo ni la wizara na akienda wizarani anaambiwa ni la Tamisemi.
Msafiri Mtakatifu alisema kwa wakati huu kipaumbele kinachopaswa kutiliwa mkazo zi barabara za juu wala ununuzi wa ndege bali ni elimu kwanza mambo mengine yafuate baadae. Gilbert Nelson alisema ili kuinua elimu inatakiwa wizara hiyo kutengewa bajeti ya kutosha na kuwepo na uwekezaji mkubwa kama serikali inavyofanya katika maeneo mengine.
"Hatuwezi kuingia katika uchumi wa maendeleo ya viwanda bila ya kuwa na watu wenye elimu" alisema Nelson. Mwaka 2016/2017 katika bajeti ya Wizara ya Elimu iliidhinishwa shilingi bilioni 277 sawa na asilimia 31 ilikadiriwa kukusanywa kutoka kwa wahisani na washirika wa maendeleo.
Katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 serikali imekadiria kukusanya kutoka kwa wahisani na washirika wa maendeleo shilingi bilioni 310 sawa na asilimia 33.7 ya fedha ya maendeleo ikiwa ni ongezeko la utegemezi kwa asilimia 10.6.
Wadau wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Uchambuzi wa bajeti hiyo ukiendelea.
Mzee Hamisi Katumwa akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Mdau Msafiri Mtakatifu akichangia jambo.
Mdau Wilfred akichangia jambo kuhusu bajeti hiyo.
Bi. Ester Tibaigana akichangia jambo.
Muonekano wa chumba cha mkutano huo wakati wa uchambuzi wa bajeti hiyo.
Bi. Marytaus Mbawala akichangia mada.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment