Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipandikilo kilichopo katika Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Lazaro Kagundulilo (kulia), akizungumza na wanahabari pamoja na wataalamu wa kilimo kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na , Jukwaa la Bioteknojia na Uhandisi Jeni (OFAB), wilayani humo jana. Wataalamu hao wa kilimo wapo katika wilaya hiyo kwa ziara ya kutoa mafunzo ya kilimo chenye tija kwa maofisa ugani wa Mkoa wa Geita.
Maofisa ugani wakiangalia eneo ambalo patalimwa shamba dogo la mfano katika Kijiji cha Kibehe Kata ya Kigongo.
Na Dotto Mwaibale, Chato
MBEGU bora za zao la mhogo
zinazositahimili magonjwa ya Batobato na michirizi kahawia zinahitajika
ili kuweza kunusuru kukumbwa na baa la njaa kwa wakulima wa zao hilo
katika Wilaya ya Chato mkoani Geita baada ya mbegu walizolima msimu huu
kushambuliwa na magonjwa.
Wananchi wa wilaya hiyo wanategemea
zaidi zao la mhogo kama chakula chao kikuu pamoja na biashara lakini
hivi sasa hali siyo shwari kutokana na mihogo waliyopanda kushambuliwa
na magonjwa.
Akizungumza na wataalamu wa kilimo kutoka Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia na watafiti wa kilimo kutoka Jukwaa la
Bioteknolojia Tanzania (OFAB), walio katika ziara ya kutoa mafunzo ya
kilimo chenye tija wilayani humo leo, mkulima wa zao la mhogo katika
Kijiji cha Ipandikilo, Andrew Misano alisema changamoto kubwa waliyonayo
ni magonjwa yanayoshambulia zao hilo.
Misano alisema msimu wa
mwaka huu umekuwa tofauti na misimu mingine kutokana na zao la mhongo
kushambuliwa na magonjwa ya batobato na michilizi kahawia. "Msimu huu
nimelima ekari saba za mhogo lakini sitegemei kuvuna chochote kutokana
na kushambuliwa na magonjwa hayo" alisema Misano.
Misano alisema
kukosekana kwa mbegu bora na inayostahimili magonjwa kumechangia
wakulima kuwa na changamoto ya zao hilo katika maeneo mengi ya wilaya
hiyo.
Kaimu Ofisa Kilimo na Umwagiliaji wa Wilaya ya Chato,
Faidaya Isango alisema zao la mhogo katika wilaya hiyo limeshambuliwa na
magonjwa kwa zaidi ya asilimia 60 katika Tarafa za Kechumba, Namilembe
na Busilayombo ambapo ameeleza kuwa isipopatikana njia mbadala ipo
hatari ya kuwepo uhaba mkubwa wa chakula.
Alisema changamoto
nyingine kubwa iliyopo ni kwa wakulima kuendelea kung'ang'ania mazao ya
mihogo iliyoshambuliwa na magonjwa badala ya kuing'oa kama
wanavyoshauriwa na maofisa ugani ili isisambaze ugonjwa katika maeneo
mengine.
Alisema kunasheria zimeandaliwa kwa ajili ya kuwabana
wakulima wakaidi na zipo katika hatua ya kuanza kufanya kazi baada ya
kupitishwa rasmi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipandikilo Lazaro
Kagundulilo alisema awali katika ekari tatu za mhogo kabla ugonjwa huo
haujaanza walikuwa wakivuna magunia zaidi ya 25 lakini hivi sasa
hawategemei kupata hata magunia matano jambo ambalo ni changamoto kubwa
kwao.
Mtaalamu wa mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha
Ukiliguru Dk.Jeremiah Simoni alisema njia mbadala ya kuwasaidia wakulima
hao ni kuanzisha mashamba darasa ambayo yataweza kutoa mbegu safi
ambazo hazina magonjwa ya Batobato na michilizi kahawia kutokana na
magonjwa hayo kutokuwa na dawa mbadala.
Mtaalamu wa masuala ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiliguru jijini Mwanza, Dk. Jeremiah Simon (kulia), akitoa maelezo kwa wanahabari wakati walipotembelea moja ya shamba la zao la mhogo lililokumbwa na ugonjwa wa batobato na michirizi ya kahawia wakati wa ziara hiyo katika Kijiji cha Ipandikilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipandikilo kilichopo katika Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Lazaro Kagundulilo, akiwaonesha waandishi wa habari shina la mhogo lililoathiriwa na magonjwa.
Ofisa Program wa OFAB kutoka Shirika la AATF la nchini Kenya, Suleiman Okoth (kushoto), akiwaelekeza jambo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ipandikilo, Clara Fidelis (kulia) na Ofisa Ugani wa Wilaya ya Chato, Charles Ntaki.
Shamba la mhogo lililoathiriwa na magonjwa.
Wanahabari wakitoka shambani.
Wakulima wa Kijiji cha Ipandikilo wakimenya mihogo tayari kwa kuianikwa kwa ajili ya unga wa ugari. Kutoka kulia ni Veronica Zakaria, Joyce Joseph na Teloza Lugiyege.
Shamba la mhogo linaloonekana kustawi vizuri lakini tayari limeathiriwa na magonjwa ya batobato na mchirizi kahawia.
Mkulima Andrew Misano akitoa maelezo kwa wanahabari kuhusu changamoto mbalimbali za kilimo cha mhogo.
Mtaalamu wa masuala ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiliguru jijini Mwanza, Dk. Jeremiah Simon (kushoto), akizungumza na wakulima wa kijiji cha Ipandikilo kuhusu mbegu bora za mhogo.
Mjumbe wa Kijiji cha Idoselo, Majeshi Mussa akiwaonesha waandishi wa habari mtama ulioathirika kwa kukosa mvua.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
No comments:
Post a Comment