Na Mathias Canal, Dar es salaam
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Taifa kwa kutekeleza sera na kuisimamia ilani ya ushindi ya CCM ya mwaka
2015/2020 na kuwaomba watanzania wote kwa kauli moja pasina itikadi za
vyama kumuunga mkono kwani atakuwa imara na madhubuti zaidi katika
utendaji wake iwapo ataungwa mkono na watanzania wote.
Chama
cha Mapinduzi (CCM) Kimetoa pongezi hizo kutokana na maamuzi
yaliyofanywa na Rais Magufuli mara baada ya kupokea Ripoti ya kamati
iliyokuwa inachunguza Hatma ya mchanga wa madini iliyoundwa na Rais
Magufuli Machi 29 mwaka huu ikiwajumuisha Profesa Abdulkarim Hamisi
Mruma (Mwenyekiti), Profesa Justiania Rwezaura Ikingula, Profesa Joseph
Bushweshaiga, Dokta Yusuph Ngenya, Dokta Joseph Yoweza Phili, Dokta
Ambrose Itika, Mohamed Zengo Makongoro na Hery Issa Gombela.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM,
Itikadi na Uenezi Ndg Humprey Polepole wakati akizungumza na Waandishi
wa Habari katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini
Dar es salaam.
Polepole
alisema kuwa uamuzi wa kuundwa kwa kamati hiyo ulitokana na kukamatwa
kwa makontena 277 ya mchanga huo katika bandari ya Dar es salaam Machi
23 Mwaka huu baada ya Rais kufanya ziara ya kushitukiza katika bandari
hiyo na kukuta makontena 20 yakiwa mbioni kusafirishwa kinyume cha
maelekezo yake ya Machi 2 ya kuzuia kusafirisha mchanga huo nje ya nchi.
Alisema
kuwa huu sio wakati wa kulumbana na kutofautiana kisa itikadi za vyama
bali ni wakati wa kusimama pamoja na kuikabili vita ya kiuchumi kwani
kwa kuzingatia taarifa iliyosomwa na Profesa Mruma mbele ya Rais
Magufuli imebainisha jinsi Taifa lilivyopata hasara ya mabilioni ya
fedha kwa kuwa makontena yaliyozuiliwa bandarini yana thamani ya madini
yaliyomo kwa kiwango cha wastani wa shilingi Bilioni 829.4 na kiwango
cha juu ni Shilingi Trioni 1.4
"Tumeibiwa
na kudhulumiwa sana mali zetu ambazo tumezirithi kutoka kwa babu zetu
lakini awamu ya Tano ikiongozwa na Rais Magufuli imeamua kwa dhati
kabisa kutilia mkazo Vita dhidi ya Rushwa, Uhujumu uchumi, Udhalimu wa
kila namna, sambamba na wizi na ufisadi kwa maslahi mapana ya Taifa la
Tanzania na Watanzania wote" Alisema Polepole
Akizungumzia
Mauaji yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini hususani Mkoani
Pwani katika Wilaya ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga alisema kuwa kipindi
hiki kigumu kwa kuwapoteza ndugu zetu vyama vya siasa vilipaswa
kushikamana kwa pamoja pasina kujali itikadi zao badala yake vimeanza
kutumia misiba hiyo kwa maslahi ya kiuongozi kuliko maslahi ya Taifa.
Polepole
alisema kuwa vyombo vyote vya serikali vinavyoshughulikia ulinzi
vinapaswa kutumia Rasilimali zao, Weledi na Utendaji wao, na kuweka
umaalumu katika kuyakabili matukio ya mauaji na kuyakomesha kabisa.
"Hakuna
dini yoyote Duniani inayoamini katika kutoa uhai wa mtu ambapo pia kuua
mtu ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo
Tunataka amani ya wananchi wetu inarudi"
"Tunatambua
kuwa wananchi wetu wanapita katika wakati mgumu kutokana na kukatishwa
kinyama maisha ya Wananchi wenzao, Viongozi, Askari, Watendaji wa
serikali, Wanachama wa CCM si kwa sababu ya mapenzi ya Mungu Bali kwa
sababu yamekatishwa katika namna inayokiuka ubinadamu kwa kuuawa
kikatili na watu wasio na Utu, Hisia na Imani ya Dini" Alisema Polepole
Polepole
ametilia msisitizo wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi kuhusu
watu wanaofanya mauaji hayo kwani ushirikiano huo utasaidia kufichua
uovu wa wadhalimu wanaokatisha maisha ya watanzania.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Itikadi na Uenezi Ndg Humprey Polepole wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es salaam.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Itikadi na Uenezi Ndg Humprey Polepole akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es salaam.
MWISHO
No comments:
Post a Comment