Saturday, April 22, 2017

NAIBU KATIBU MKUU NISHATI NA MADINI ATEMBELEA MIRADI YA TANESCO KINYEREZI




NA MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt, Juliana Palangyo, (pichani anayezungumza), ametembelea miradi ya kuzalisha umeme wa Gesi Asilia ya upanuzi wa Kinyerezi I pamoja na ule wa Kinyerezi II.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua miradi hiyo, Dkt Pallangyo ameridhishwa sana na jitihada zinazofanywa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), katika kuhakikisha Miradi hiyo inakamilika kwa wakati, ambapo mpaka sasa ujenzi wa mradi wa kinyerezi II umefikia asilimia 53%.

“Niwapongeze sana TANESCO kwa jitihada kubwa mnazozifanya katika kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati, ambapo mmewezesha Majenereta 8 yenye jumla ya Megawati (MW) 240 mpaka sasa yameshafika, hii ni hatua nyingine kubwa sana ,hivyo kupitia Mradi huu wa kinyerezi nina amini Tanzania ya Viwanda inawezekana”.

Akielezea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kinyerezi II, Meneja wa Kituo hicho Mhandisi Steven Manda alisema kuwa kituo hicho kinaendelea vizuri na ujenzi katika kuhakikisha kinakamilika Desemba 2018, ambapo mpaka sasa ukamilifui wa Mradi huo unategemea Kinyerezi I kutokana na Baadhi ya mitambo kuingiliana hasa mitambo ya mfumo wa upozaji maji ambao utaunganishwa na mtambo wa Kinyerezi I.

Naye Kaimu meneja wa Kituo cha Kinyerezi I Mhandisi Lucas Busunge amesema kuwa Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 150, Umeongezewa uwezo wa kuzalisha Megawati zingine 185 ikiwa ni Awamu ya pili ya upanuzi wa Mradi huo.

Kwa ujumla miradi yote miwili itakapokamilika, jumla ya Megawati 575MW za umeme utokanao na Gesi Asilia, zitazalishwa na kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na hivyo zitasaidia kuongeza upatikanaji wa Umeme wa Uhakika na kuwezesha wananchi wengi kupata huduma ya umeme na kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha Umeme unatumika kama njia moja wapo ya kuleta maendeleo ya wananchi na kuinua vipato vyao binafsi na Taifa kwa ujumla. Naibu waziri Pallangyo alifanya ziara hiyo Aprili 20, 2017.



Mafundi wakiendelea na kazi katika moja ya jengo lilopo katika mradi wa kufua umeme wa gesi asili megawati 240 wa Kinyerezi I ambapo unafanyiwa upanuzi.


Naibu katibu Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Juliana Pallangyo (wa pili kutoka kushoto) akiambatana na viongozi wa TANESCO alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Miradi ya Umeme Kinyerezi I&II. Kulia kwake ni kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bi.Joyce Ngahyoma akifuatiwa na Kaimu Meneja Uhusiano Bw. Yasini Didas Slayo Kulia pamoja na Meneja Mradi wa Kinyerezi II, Mhandisi Stephen Manda, (Kushoto)

No comments:

Post a Comment