Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Mzee John Samwel Malecela akizungumza wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Na Mathias Canal, Dodoma
Askari na Maafisa wa jeshi la Polisi
nchini wameaswa kutotumia madaraka yao vibaya kwa kuwabambikizia
wananchi kesi kwani kufanya hivyo ni kushindwa kusimamia dhamira njema
ya Mhe Rais ya kuwapatia wananchi wanyonge haki zao stahiki.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe Mwigulu Nchemba
wakati akifungua kikao cha kazi cha Siku tatu cha mwaka 2017 kwa maafisa
waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi kilichofanyika katika
ukumbi wa Mikutano wa LAPF Mjini Dodoma.
Mhe Mwigulu amesema
kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kuwabambikizia
kesi, Kuwabadilishia watu kesi zao za msingi kwa sababu ya kushindwa
kutoa rushwa hivyo kikao hicho kinapaswa kuwa na maamuzi na maadhimio
yenye dira na taswira njema kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza
pia Askari na Maafisa wa Polisi kutotumia taarifa za watu wanaohasiana
kuwa ndio chanzo pekee cha msingi wa shtaka badala yake kufanya
uchunguzi kwa kina na kujiridhisha vyema ili kufikia hukumu yenye tija
Na haki kwa mtuhumiwa kwani kufanya hivyo kutaimarisha amani na jeshi la
Polisi kupata taarifa nyingi za uhalifu kutoka kwa wananchi endapo
watajikita katika haki.
Akizungumzia Vita dhidi ya Dawa za
Kulevya Mhe Nchemba alisema kuwa serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kukamata na kuziteketeza Dawa za kulevya zilizopo mashambani ambapo
ametilia msisitizo zaidi kwa Askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi
kuendelea kupambana ili kuzikamata Dawa za kulevya zilizopo katika
viwanda.
Amesisitiza pia Jeshi la Polisi kuendelea kupambana na
kubaini uhalifu sambamba na kushirikiana na vyombo vingine ili
kuhakikisha lengo mahususi la serikali ambalo ni kuzuia uhalifu
linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mhe Mwigulu amesema kuwa kauli
mbiu ya Mwaka 2017 inayosema "ZINGATIA MAADILI TUNAPOPAMBANA NA UADILIFU
ILI KUIMARISHA USALAMA KWA MAENDELEO YA TAIFA" endapo kama itatekelezwa
kwa vitendo itaijenga nchi na kuzidi kudumisha zaidi amani iliyopo kwa
wananchi.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu
alisema kuwa kikao hicho cha kazi kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi kina
dhamira kubwa ya kufanya Tathmini ya utendaji wa mwaka 2016 na kuandaa
mikakati mizuri ya mwaka 2017 na kupata fursa ya kubadilika kiutendaji
kwa kuzingatia dhamira ya serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe
Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Hata hivyo amesisitiza zaidi askari
wote nchini kutofanya kazi kwa mazoea, Kuacha Urasimu na kujenga
uaminifu na weledi katika kazi.
Mangu amesema matendo ya Askari
Polisi nchini yanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii hivyo
askari Polisi hapaswi kuwa chanzo cha vurugu au kujihusisha na matendo
ovu yasiyostahili katika jamii.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo
yatakayopewa kipaombele kwa kujadiliwa katika Kikao hicho itakuwa ni
pamoja na Vita dhidi ya Dawa za Kulevya, Vita dhidi ya Magendo, Vita
dhidi ya ujangili na Uvuvi sambamba na Vita dhidi ya Ubambikizaji wa
kesi kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe
Jordan Lugimbana akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma kabla ya kumkaribisha
Waziri Mwigulu Nchemba kuzungumza na askari hao amelipongeza jeshi la
Polisi kwa kazi kubwa linayofanya ambapo pia ameeleza mpango wa Mkoa
katika kupambana na migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kamati maalumu ya
wataalamu wa sheria kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Kupitia na
kushauri ili kuweza kumaliza haraka migogoro hiyo.
Naye Makamu wa
kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel Malecela alisema
kuwa jambo la msingi ambalo askari Polisi wanapaswa kulifanya ni pamoja
na kuhakikisha kila mwananchi anapata Uhuru wake na kama jambo hilo
likitekelezwa ipasavyo Fikra za Hayati Mwalimu J.K Nyerere zitakuwa
zimeenziwa kwa weledi.
Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
SACP Ramadhani Mungi Msimamizi wa bandari Tanzania na Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi Renata Mzinga wakifatilia kwa makini kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel Malecela mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu Akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Lugimbana akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
No comments:
Post a Comment