Monday, May 23, 2016

SERIKALI KUJENGA NYUMBA 9500 KWA AJILI YA ASKARI MAGEREZA

Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
Serikali kupitia jeshi la Magereza imesaini Mkataba na Kampuni ya Poly Technologies ya China kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya Magereza nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni wakati akijibu swali kuhusu kuboresha makazi ya askari lililoulizwa na Mhe. Devota Minja (Mb) leo bungeni mjini Dodoma.
Mhe. Masauni alibainisha kuwa kupitia mkataba huo Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto iliyopo ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya askari wa jeshi hilo ambapo mahitaji kwa sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221 hivyo kupelekea upungufu wa nyumba 10,279.

“Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi, hivyo katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na pia kujenga nyumba mpya”. Alisema Masauni.

Mhe. Masauni alifafanua kuwa mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo mpya ni Makao Makuu ya Magereza nyumba 472, Arusha nyumba 377, Dar es Salaam nyumba 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani nyumba 84.

Aidha, Mhe. Masauni aliongeza kuwa kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar zitakazosaidia kupunguza tatizo la makazi kwa askari wa jeshi hilo.

Mhe. Masauni alilieleza bunge kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika.





No comments:

Post a Comment