Thursday, May 19, 2016

KATIBU MKUU AFANYA ZIARA YA GHAFLA BANDARINI KATIKA MITA ZA KUPIMA MAFUTA

Na. Lorietha Laurence -  Maelezo,Dar es salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi) Mhandisi Dkt. Leornad Chamuriho ameupa siku mbili uongozi wa Bandari unaosimamia Mita ya Kupimia mafuta nchini (Flow Meter) iliyoko Kigamboni jijini Dar es salaam kuhakikisha kuwa unatoa taarifa ndani ya siku mbili kuhusu hitilafu iliyojitokeza kwenye mfumo wa kufungua valvu za mita hiyo upande wa umeme. 

Aidha, ameuagiza uongozi huo kutoa taarifa kuhusu hitilafu ya kamera 2 za usalama zilizoungua na kushindwa kufanya kazi kwa takribani mwezi mzima. 

Katibu Mkuu huyo ametoa maagizo hayo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mita hiyo eneo la mji Mwema Kigamboni leo jijini Dar es salaam na kubaini upungufu wa utendaji wa baadhi ya maeneo.

Maeneo hayo ni pamoja na  kamera za kufuatilia mwenendo wa usalama wa mita hiyo, valvu zilizoshindwa kufanya  kazi upande wa mfumo wa umeme hivyo kubakiwa na njia ya analoji kutokana na hali ya mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha jijini Dar es salaam. 


“Ifikapo Jumatatu nipatiwe taarifa kuhusu matengenezo ya vifaa hivi, hatua zilizochukuliwa na mnieleze lini ukarabati wake utakamilika pia ujenzi wa paa kuzuia athari ya mvua kwenye mita hii” amesema Dkt. Chamuriho.

Ameongeza kuwa dhumuni la Serikali ni kuhakikisha vifaa hivyo vinafanya kazi katika viwango vinavyostahili ili kulinda mapato yanayotokana na mafuta yanayoingia nchini ili Serikali ipate kodi halali na hivyo kuongeza mapato ya nchi na kuondoa malalamiko kwa wateja.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mita hiyo  kutoka Mamlaka ya  Bandari nchini Mhandisi Mary Mhayaya ameeleza kuwa uharibifu wa vifaa hivyo umesababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na tayari vifaa hivyo vimeanza  kukabarati.

" Kisichofanya kazi ni mfumo wa kufungua mafuta upande wa umeme kwenye baadhi ya valve, upande wa analoji unafanya kazi vizuri na kazi ya upakuaji mafuta kupitia mfumo wa analojia inaendelea kama kawaida" Amesisitiza.

Amesema kuwa tayari wamemweleza mkandarasi aliyefunga vifaa hivyo kuvifanyia marekebisho haraka iwezekanavyo.
Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Hebel Mhanga amesema kuwa ofisi yake inajukumu la kuhakikisha inatoa huduma sahihi kwa wateja wanaotumia mitambo hiyo iliyopo bandarini  hapo na Serikali inapata mapato kulingana na huduma iliyotolewa.

Mita ya Kupimia Mafuta yalnayoingia nchini iko katika hatua ya majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo tayari meli tatu zimefanyiwa majaribio ya upakuaji wa mafuta huku moja ikiwa imefanyiwa vipimo.




No comments:

Post a Comment