Tuesday, November 03, 2015

FAINI ZILIVYOSAIDIA KUPUNGUZA MAKOSA YA UKATILI WA JINSIA MASOKONI

FAINI zinazotolewa kwa watu wanaobainika na makosa ya unyanyasaji wa kijinsia katika soko la Gezaulole lililopo Kiwalani Bomubomu Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam zimesaidia kupunguza vitendo hivyo kwenye soko hilo

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam leo asubuhi na Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Khadija Mohamed wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari waliotembea soko hilo kujua ni kwa kiwango gani vitendo hivyo vimepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa elimu ya kupinga unyanyasaji katika masoko ya Manispaa ya Ilala
"Faini tunazo watoza wafanyabiashara wanaobainika na makosa ya kutumia lugha chafu, kupigana na kuwadhalilisha wenzao kwa kuwakamata  maunguni na unyanyasaji mwingine zimesaidia kupunguza makosa hayo katika soko letu" alisema Mohamed.

Alisema mara zote matusi katika masoko yamekuwa yakichangia kuwakimbiza wateja na ndio maana wana lishukuru shirika la EFG kwa kuwapa elimu iliyowasaidia na kuwafanya waendelee na biashara zao kama kawaida
Mwezeshaji wa Sheria Amina Mussa alisema hapo awali wanaume walikuwa wamekubuhu kwa kutukana tusi la mama jambo ambalo lilikuwa linawakera lakini hivi sasa wanashukuru mungu baada ya wanaume hao kujitambua na kuacha matusi hayo

Mwenyekiti wa soko hilo, Muhidin Waziri alilipongeza shirika hilo kwa kuwasaidia wafanyabiashara katika masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala na kujitambua hivyo kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia masokoni.

Katibu wa soko hilo, Salum Yusuf(PICHANI JUU) alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo hapo awali kabla ya kufikiwa na EfG ilikuwa ni kutojua maana ya unyanyasaji ambapo mtu aliyekuwa akishikwa mwilini au kutukanwa alikuwa hachukui hatua yoyote

Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika hilo, Samora Julius alitoa ushauri kwa Serikali hasa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ukatili wa jinsia

Julius aliomba serikali kuyaunga mkono mashirika yanayofanya vizuri kwa kuyapa ruzuku itakayosaidia kuwafikia wananchi kwa wingi na jamii kwa ujumla.




Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika hilo, Samora Julius akitoa ushauri kwa Serikali hasa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ukatili wa jinsia. Kushoto ni mtaalamu wa kujitolea wa masuala ya kijinsia kutoka nje ya nchi,



Mwezeshaji wa Sheria, Khadija Mohamed (kulia), akielezea mafanikio waliyoyafikia ya kukabiliana na vitendo hivyo katika soko hilo baada ya kuwezeshwa na EfG.



Mfanyabiashara wa samaki katika soko hilo, Asha Mohamed akihojiwa na wanahabari kuhusu namna wanavyo pambana na ukatili katika soko lao hilo la Gezaulole.





No comments:

Post a Comment