Thursday, October 08, 2015

KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA TAKWIMU

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (PICHANI KUSHOTO) amewataka watendaji wa Serikali kutoa takwimu mbalimbali za maendeleo na kuziweka katika mitandao ili wananchi waweze kuziona na kuhoji mipango ya maendeleo iliyofanyika au kukwama.

Amebainisha hayo leo wakati akifungua mkutano wa wadau wa takwimu ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dar es Salaam leo kwa lengo kukubaliana jinsi ya kushirikiana katika kuhakikisha takwimu za viashiria vya Mpango wa Maendeleo Endelevu zinapatikana kwa wakati.

Amesema takwimu mbalimbali ni lazima zioneshe mipango ya maendeleo iliyofanyika au kumalizika badala ya kuwa siri na kuwafanya wananchi kushindwa kuhoji.

"Takwimu mbalimbali za maendeleo zikiwa wazi itasaidia wananchi kufahamu miradi ya maendeleo iliyopo na iliyokwama jambo ambalo litasaidia kusukuma maendeleo ya nchi" anaeleza Sefue.


Amesema lengo la lengo la kuelimishana juu ya kukamilika kwa utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) na kuanza kwa Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu - Sustainable Development Goals (SDGs).

Anaongeza kuwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia - MDGs ulikuwa ni wa miaka 15 kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.

Mpango huu wa MDGs unakamilika mwaka huu na kuanza kwa mpango mpya wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambao pia ni miaka 15 ijayo.

Amesema Tanzania ni nchi ya kwanza kuanza kufanya vikao vya kutekeleza mpango huo wa maendeleo jambo ambalo linaonesha kuwa na kasi ya kuyafikia maendeleo hayo ya dunia.

Mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umehudhuriwa na wadau wa takwimu takribani 100 kutoka Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Wadau wa Sekta Binafsi pamoja na Wadau wa Taasisi za Elimu ya Juu.

Septemba mwaka huu, viongozi wa nchi mbalimbali duniani akiwemo Rais Jakaya Kikwete walikutana nchini Marekani kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia – MDGs ambapo ilionekana kwamba kuna baadhi ya malengo yalikuwa yamefanikiwa na mengine hayakufanikiwa.





Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk.Albina Chuwa akihutubia kwenye mkutano huo.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Profesa Adolph Mkenda akizungumza katika mkutano huo.



Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Dk.Rogers Dhliwayo akizungumza kwenye mkutano huo.



Washiriki wakiwa katika mkutano huo leo.





No comments:

Post a Comment