Monday, September 21, 2015

MASABURI:LOWASSA NDIYE ALIYEUZA UDA

MGOMBEA wa ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Didas Masaburi, amekana kuhusika na uuzwaji wa mali za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na kutupa mzigo huo kwa mgombea wa urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa.
Dkt. Masaburi amedai kushangazwa na kauli zinazotolewa na wapinzani wake hasa wa vyama vya upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakimtuhumu kuhusika kwake na uuzwaji wa mali za UDA wakati si kweli.

Akizungumza katika kampeni zake zilizofanyika Kata ya Makuburi juzi, Dkt. Masaburi alidai Lowassa akiwa Waziri Mkuu ndiye aliyehusika na uuzwaji wa UDA kwani alisimamia kwa kina kuhakikisha hilo linafanikiwa.

“Kipindi mimi nilipokuwa meya (wa Dar es Salaam) nilikuta tayari aliyekuwa waziri mkuu kipindi hicho Edward Lowassa amesaini mikataba ya uuzaji wa hisa za UDA, sasa nani fisadi hapa?” Alihoji.
Dkt. Masaburi alidai, wakati akiwa meya aliikuta Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa inamiliki mali nyingi, lakini wajanja walikuwa wakifaidika binafsi ndipo alipoamua  kupitia mikataba yote na kubaini ubadhirifu huo wa UDA.

“UDA iliuzwa kwa kampuni ya Simon Group kwa Sh milioni 285, lakini nilipohoi kuhusu hizo fedha nikaambiwa zipo Sh milioni 85 na Sh milioni 200 hazijulikani zilipo, niliamua kuivunja bodi ya shirika hilo na kuwasimamisha kazi baadhi ya watendaji ili kupisha uchunguzi,” alisema.

Alifafanua kuwa, wakati hisa za UDA zinauzwa mwaka 2008 hakuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam na alipoingia ndipo alipokuta uozo mwingi na kuanza kusafisha baadhi ya mambo.

“Kumekuwa na wimbi kubwa la wagombea wanaotumia vibaya majina ya vyama au wagombea wengine kuwachafua ikiwa  ni moja ya sera zao wanapopanda majukwaani, wanasahau kuwa miongoni mwa watu wanaowasema ni viongozi wao wenyewe,” alisema.

Dkt. Masaburi alisema, endapo atachaguliwa kuliongoza jimbo hilo atahakikisha anashirikiana na Serikali katika kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo  barabara za ndani ya  mitaa kwa kiwango cha lami, kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana na kuongeza ajira kwa vijana  kupitia mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) na miradi mingine.

Alisema moja kati vipaumbele vyake ni kuboresha elimu na vituo vya afya, kurekebisha mifumo ya majitaka pamoja na kuwatengea wanawake na watu wa makundi maalumu mfuko utakaowawezesha kukopa.


No comments:

Post a Comment