Friday, July 10, 2015

OKWI RASMI SONDERJYSKE FC


Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi amesaini mkataba wa miaka mitano katika klabu ya SonderjyskE FC ya Ligi Kuu ya Denmark.

Katika klabu hiyo Okwi atakuwa analipwa dola za Kimarekani 10,000 kwa mwezi, akipatiwa nyumba, usafiri na huduma nyingine zote muhimu Denmark.

Katika Tovuti ya klabu hiyo imesema makubaliano baina ya Okwi na klabu yake ya zamani, Simba yamekamilika na sasa taratibu za usajili zinaendelea baada ya juzi kukabidhiwa jezi namba 25 aliyokuwa anatumia Tanzania.

Kocha Hans Jorgen Haysen alisema kwamba Okwi ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa, kasi, nguvu na utaalamu wa hali ya juu.

BOFYA CHINI KUSOMA ZAIDI

“Ana jina kubwa sana Tanzania na Uganda, ambako ameonyesha umahiri wake mkubwa wa kufunga katika klabu na timu ya Taifa,”alisema kocha huyo.

Okwi aliyeifungia mabao 18 timu ya Taifa ya Uganda katika mechi 35, msimu uliopita aliichezea Simba akitokea kwa mahasimu wao Yanga ambako pia alicheza kwa nusu mwaka kabla ya kutofautiana na viongozi wa klabu hiyo na kuondoka.

Simba ndiyo iliyomuingiza Tanzania Okwi mwaka 2010 akitokea SC Villa ya kwao. Alicheza Msimbazi hadi mwaka 2013 aliponunuliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola za Kimarekani 300,000 (Sh. Milioni 600 na zaidi).

Hata hivyo, Okwi aliondoka Tunisia baada ya miezi mitatu kufuatia kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo na baadaye kufungua kesi FIFA akiomba aruhusiwe kucheza klabu nyingine kulinda kipaji chake wakati mgogoro wake na Etoile unaendelea.

Etoile ilisitisha huduma kwa Okwi, baada ya kukerwa na desturi ya mchezaji huyo kuchelewa kurejea kujiunga na timu anaporuhusiwa kwenda kujiunga na timu yake ya Taifa Uganda.

Akasaini tena SC Villa katikati ya mwaka 2013 kabla ya Desemba mwaka huo, kuhamia Yanga wakati wote huo kesi yake na Etoile ikiendelea FIFA.

Hata hivyo, Agosti mwaka jana, Okwi akarejea Simba kwa Mkataba wa miaka miwili kabla ya mwezi huu kuhamia Denmark.

Etoile haikuwahi kuilipa Simba fedha za manunuzi ya Okwi na klabu ya Tanzania ilifungua kesi FIFA ikashinda, timu ya Tunisia ikiamriwa hadi katikati ya mwaka jana, lakini hadi leo haijafanya hivyo.

Simba inaweza kupoza machungu iwapo SonderjyskE FC itatoa dau zuri, ambalo hadi sasa ni siri yao.

No comments:

Post a Comment