Tuesday, June 09, 2015

KOCHA YANGA AANZA TAMBO KUELEKEA KAGAME


KOCHA Mkuu wa Yanga Hans Van de Pluijm amesema atahakikisha Kombe la Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kagame linabaki mikononi mwao kwa jinsi anavyokiamini kikosi chake.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai,mwaka huku Tanzania wakiwa wenyeji wa michuano hiyo.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyoanza rasmi leo katika Uwanja wa Karume, Pluijm alisema kuwa timu yake imeanza mazoezi kwa kasi ili kujiweka tayari na mashindano hayo.

Watatumia michuano hiyo kudhihirisha ubora wa kikosi chao pamoja na kujiandaa kwa msimu ujao wa ligi kuu.

"Tumeanza mazoezi ya nguvu ili kuhakikisha tunafanya vizuri katika michuano hii ya Kagame na kombe kubaki nyumbani ili kuendeleza ushindi ndani ya timu yetu," alisema Pluijm.

Alisema pia watatumia michuano hiyo ili kujiweka sawa katika msimu ujao wa ligi kuu na kuhakikisha wanaendelea kutetea ubingwa wa Bara.

BOFYA CHINI KUENDELEA...


"Tutatumia michuano hii kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi, kwani malengo ya kikosi changu ni kuhakikisha tunaendeleza mbio za ushindi ili kuwapa raha mashabiki na wanachama wa Yanga," alisema Pluijm.

Kwa upande wa usajili Pluijm alisema kuwa amefarijika kuona uongozi wa timu hiyo umetekeleza maombi yake kwa kusajili wachezaji aliokuwa anawataka.

Usajili huo utaifanya Yanga kuwa timu tishio katika msimu ujao wa ligi kuu na kuchukua ubingwa mapema zaidi kuliko ilivyokuwa kwa msimu uliomalizika.

Wakati huo huo mchezaji wa timu hiyo Said Makapu ameanza mazoezi mepesi ili kujiweka sawa kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.

Pluijm alisema kuwa hadi kufikia wiki ijayo mchezaji huyo atakuwa ameshapata nafuu na kuweza kushiriki mazoezi rasmi.


No comments:

Post a Comment