Wednesday, May 28, 2014

MAPATO MALAWI Vs TAIFA STARS AIBU TUPU, STARS KUELEKEA HARARE KESHO

Wachezaji wa Tanzania, Taifa Stars wanatarajiwa kuondoka kesho (mei 29)  ikiwa ni msafara wa watu 30 unaojumuisha na benchi la ufundi na viongozi kuelekea Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.

Mechi hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa mjini Harare wakati Taifa Stars itatua jijini humo saa 5 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.

Msafara wa Taifa Stars ambayo ambayo jana (Mei 27 mwaka huu) ilicheza mechi ya kujipima nguvu na Malawi na kushinda bao 1-0, na utarejea nchini Juni 2 mwaka huu unaongozwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Wakati huo huo, mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.

Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08, gharama za kuchapa tiketi sh. 225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24, gharama za mechi sh. 1,375,218.98 na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 4,469,461.69.

Katika hatua nyingine, Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Chama cha Soka Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso Mwale.

Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha Mwale, na kuongeza kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano wa kuigwa kwa makocha wazalendo waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.

Rais Malinzi amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mwale, na kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwao.

Mwale (51) alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha katika barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini kujiunga na timu yake kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory Coast.


No comments:

Post a Comment