Watu 21 wamefariki dunia katika ajali mbaya
iliyotokea jana saa mbili usiku katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani
ikihusisha magari 3 na wengine 11 kujeruhiwa.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu jana,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Ulrich Matei, alisema ajali hiyo imetokea
katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Lindi, eneo la Ikwiriri, wilayani humo.
Awali ajali hiyo ilihusisha magari mawili, Toyota
Hiace (T 948 CUX), iliyokuwa ikitokea Ikwiriri kuelekea Rufiji ambalo
lilikwenda kukwaruzana na Lori(T 132 AFJ) kwa nyumba, ambalo lilikuwa
limeharibika na kusimama barbarani.
SOMA ZAIDI . . .
Alisema baada ya kulikwaruza roli hilo, mlango wa
Hiace uling'oka na kubaki kwenye roli ambapo gari hiyo lilipoteza mwelekeo na
kwenda kugongana uso kwa uso na gari nyingine aina ya Canter(T 774 CJW) na
kupinduka.
"Katika ajali hii, watu 14 walifariki dunia
papo hapo, wakati polisi na baadhi ya wananchi wakiendelea kuwaokoa majeruhi
ili wakimbizwe hospitali, likatokea basi la kampuni ya Mining (President)( T
242 BXA), kuwakanyaga watu waliokuwa wakitoa msaada na kuwaua ndio maana idadi
ya waliokufa imefikia 21.
"Basi hili lilikuwa linatoka Lindi kuelekea
Dar es Salaam...polisi walifanya jitihada za kulisimamisha lakini dereva wake
alikataa kusimama na kwenda kukanyaga watu lakini tayari tumemkamata, majeruhi
mmoja amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam," alisema
Kamanda Matei.
Kamanda Matei alisema, basi hilo linashikiliwa
polisi ambapo uchunguzi ukikamilika, dereva wake atafikishwa mahakamani kujibu
mashtaka.
Aliwataja waliokufa ni Sixtus Ally Mtanga(32) na
Nassoro Mohamed Kajani(20) wakazi wa Ikwiriri, Juma Said Kitambulilo(30) na
Salum Goma Makonde (50), Ustaadhi Kalilambwe(34) na Shafil Kip (30), Wasabi
Sabil(45), Ramadhani Ally (23)wote wakazi wa Mbagala.
Shabani Bakari(30) Kondakta wa Hiace, mkazi wa
Kibiti, Masud Abulal (27), mkazi wa Mkuranga, Ammi Mpemba (30)na Madadi Hassan
Mangasongo (45) wakazi wa Jaribu na Japhet Ponsian (24), mkazi wa Dar es
Salaam.
Pia yupo Said Ally China (21) mkazi wa
Kimanzichana, mkazi wa Jaribu, Abdalahaman Yusuph Kihemke(45), mkazi wa Kongowe
na Fikiri Said Sauze, mkazi wa Vikindu.
Wengine ni Nywari Mshigani mkazi wa Dar es Salaam,
Hassan Wasabi (18), mkazi wa Kibiti na Seleman Mcharazi (47) mwingine
aliyejulikana kwa jina moja la Mustafa, wote wakazi wa Mbagala na maiti ya
mwanamke haijafahamika jina lake.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Frank Sixmundi
(31), dereva wa gari la Maliasili Kibiti ambaye alifika eneo ili kutoa msaada
kwa majeruhi ambaye ameumia kichwani, Mohamed Salehe (49) na Charles Rogasani (23),
wote wakazi wa Kibiti na Mohamed Mengine (42), mkazi wa Dar es Salaam.
Wengine ni Mniko Magige Mango (54) na Abdalah Issa
(25) wakazi wa Mkuranga, Khalid Salum (32), mkazi wa Dar es Salaam, Ahmad
Yusuph (23), mkazi wa Kigamboni na Shomari Yusuph (42), mkazi wa
Mburahati. Majeruhi wamelazwa katika hospitali za Ikwiriri, Misheni ya
Mchukwi na wengine hospitali ya Taifa Muhimbili.
No comments:
Post a Comment