Sunday, February 16, 2014

PEMBE ZA NDOVU ZAZIDI KUNASWA NCHINI

Mtwara,

Watu watatu wakazi wa jijini Dar Es Salaam wamekamatwa na meno ya tembo katika Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara, yenye thamani ya shillingi milioni 700.

Akizungumza ofisini kwake kwa niaba ya kamada wa polisi Mkoani hapo, kaimu kamanda, Maisha Mganga, alisema mnamo Februari 14, mwaka huu majira ya saa 11.00 alfajiri katika kijiji cha Chungu kata na tarafa ya Nanyumbu, polisi wa Wilaya hiyo wakiwa katika kizuizi cha barabara ya Mtambaswala iendayo Mangaka waliwakama watuhumiwa hao.

Alisema kuwa watuhumiwa hao walitambuliwa kwa majina ya Abdallah Ngunde (40), mkazi wa Dar Es Salaam ambaye kazi yake ni dereva, Geraldat Lukas (36), naye ni dereva pia mkazi wa Kongowe jijini hapo na Boniphace Kosan (29) mkazi wa Kimara katika jiji la Dar Es Salaamu, wote kwa pamoja walikutwa na meno 58 yenye uzito wa kilogramu 130.6.

Aidha, alisema walikamatwa na meno hayo ndani ya gari yenye namba za usajili T 208 AGC aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Hilali Rashid, mkazi wa jijini Dar Es Salaam, ambapo mbinu walioitumia hao watuhumiwa ni kukata katika sakafu ya chini ya gari na kutengeneza tenki la bandia na kisha kuweka kapeti juu yake chini ya kiti cha kukalia abiria nyuma ya dereva.

Hata hivyo alisema kuwa watuhumiwa wote watatu, gari pamoja na meno hayo ya tembo, wanashikiliwa na polisi kwa hatua nyingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani mara baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.


No comments:

Post a Comment