Sunday, February 02, 2014

MOHAMMED TRANS YAUA ASKARI POLISI WATANO JANA

Dodoma. 

ASKARI watano wa Jeshi la Polisi mkoani hapa walifariki dunia papohapo baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na basi la abiria mali ya kampuni ya Mohamed Trans usiku wa kuamkia jana.

Akidhibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma David Misime aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 01/02/2014 majira ya saa sita na robo usiku katika katika kijiji cha Mtumba kilichopo kata ya Mtumba tarafa ya Kikombo manispaa ya Dodoma katika barabara kuu ya Dodoma -Morogoro.
Misime alieleza kuwa gari ndogo lenye namba T.770 ABT Toyota Corolla lililokuwa likiendeshwa na askari wa polisi wilaya ya Kongwa mwenye namba H.3783PC Deogratius Mahinyila(29) likitokea Dodoma mjini kuelekea wilayani kongwa liligongana uso kwa uso na gari lenye namba T.997 AVW aina ya Scania basi mali ya kampuni ya Mohamed trans lililokuwa likiendeshwa na Juma Mohamed (38) mkazi wa Mwanza likitokea Dar es salaam kuelekea Dodoma na kusababisha vifo vya askari hao papohapo.
Aidha aliwataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Adolf Silla (51) Mgogo,Evarist Bukombe (34) Muha, Deogratius Mahinyila (29),ambaye ni Dereva wa gari ndogo,Jackline Tesha (22) Mchaga pamoja na Jema Luvinga (20) Mhehe ambao wote walikuwa ni askari wa wilaya ya Kongwa mkoani hapa waliokuwa wakitokea katika sherehe za kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 pamoja na kuwaaga askari wastaafu. Alibainisha kuwa hakuna abiria wa basi aliyejeruhiwa katika ajali hiyo na kusema kuwa kutokana na uchunguzi wa awali uliofanywa imebainika kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari hayo.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi kwani kutokana na uharibifu ambao umetokea katika gari dogo walilokuwa wamepanda askari hao na jinsi lilivyoburuzwa na basi kwa umbali wa mita 56 kisha na kwenda kusimama umbali wa mita 97 hivyo kwa hali hiyo umbali kutoka eneo walipogongana hadi basi lilipoenda kusimama ni mita 152”alisema Misime.

Pia alisema kuwa dereva wa basi hilo alitoroka mara baada ya ajali hiyo kutokea na jeshi la polisi linaendelea kufanya juhudi za kumtafuta ili aweze kuchuliwa hatua za kisheria na kuongeza kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt,Ibenzi Ernest alibainisha kupokea miili ya marehemu hao na kusema kuwa marehemu hao walijeruhiwa vibaya kichwani na hivyo kusababisha vifo vyao.







No comments:

Post a Comment