Kibaha
(kutoka Gazeti la Majira) Katika kupambana na kuzuia ushawishi wa vitendo vya rushwa
kwa baadhi ya makondakta na madereva wa mabasi dhidi ya askari polisi
kikosi cha usalama barabarani (trafiki), jeshi la polisi mkoa wa Pwani
limepiga marufuku madereva na makondakta wa mabasi kushuka ndani ya
magari yao kwa lengo la kupeleka kadi kwa trafiki ili kukaguliwa.
Akizungumza
na majira mjini Kibaha juzi, Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha
Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Nassor Sisiwaya alisema, kumekuwepo na
malalamiko na hisia kwa baadhi ya watu ya kwamba, kondakta au dereva wa
basi anaposhuka kupeleka kadi kwa trafiki ili ikaguliwe, kadi hiyo
huishikanisha na fedha ambayo humpa trafiki kama rushwa ili asimchukulie
hatua za kisheria katika makosa ya usalama barabarani atakayokuwa
ameyatenda.
Kamanda Sisiwaya amesema, ili kuondoa mtazamo huo na
vishawishi hivyo vya rushwa amepiga marufuku dereva au kondakta kushuka
ndani ya gari kumfuata trafiki badala yake trafiki atapanda ndani ya
gari ambapo atakagua na kuuliza maswali hadharani mbele ya abiria.
"Askari
wa usalama barabarani kwa ujumla wao nchi nzima, wamekuwa
wakilalamikiwa sana kujihusisha na vitendo vya rushwa, sikatai kuwepo
kwa askari mmoja mmoja mwenye tabia hizo kutokana na tabia yake kama
binadamu, lakini sikubaliani na trafiki wote kujumuishwa katika tabia
hiyo chafu ya kuomba na kupokea rushwa ili kupindisha sheria kwani,
naamini asilimia kubwa ya askari wetu ni waadilifu katika kutekeleza
majukumu ya kazi yao na kusimamia sheria za usalama barabarani
kikamilifu" alisema Sisiwaya.
Alisema ili kuondoa hisia na dhana
potofu miongoni mwa wana jamii, amepiga marufuku katika mkoa wake dereva
na kondakta kushuka kwenye gari na kumfuata trafiki kibandani au nyuma
ya gari badala yake trafiki ataingia ndani ya gari kufanya ukaguzi na
kuhojiana na kondakta mbele ya abiria, kama ana ugonjwa wa kuomba na
kupokea rushwa, aiombe na kuipokea hadharani mbele ya abiria ambao
amewaomba kutoa taarifa sahihi na za kweli kwa uongozi wa polisi kuhusu
trafiki yeyote watakayembaini akipokea rushwa.
"Katika stendi ya
mabasi Maili Moja, Kibaha, jeshi la polisi kwa kushirikiana na kamati ya
usalama barabarani ya mkoa, tutafunga maspika makubwa ambayo yatatumika
kuwatangazia makondakta na madereva kutokushuka katika magari yao na
kuwataka wabaki ndani wakimsubiri trafiki kuwakagua ndani ya basi, mbele
ya abiria" alisema Sisiwaya.
Alisema kwamba, uongozi wa jeshi la
polisi mkoa wa Pwani, na kikosi cha usalama barabarani cha jeshi hilo
halitamvumilia askari yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya
rushwa , hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni
pamoja na kufukuzwa kazi.
"Haiwezekani jeshi zima kuchafuliwa na
watu wachache, waroho wafedha, wanaokiuka maadili ya jeshi na
kujihusisha na vitendo vya rushwa, kama wapo kweli askari wenye tabia
hizo ndani ya mkoa wa Pwani, waache mara moja kwani, viongozi wao
tumejipanga kikamilifu kuwasaka na kuwakamata kwa ushirikiano na
wananchi na pale tutakapomkamata askari kwa kuomba na kupokea rushwa,
tutamshughulikia vilivyo kwa mujibu wa sheria ili awe mfano na funzo kwa
wengine wenye mchezo na tabia hizo chafu za kuomba na kupokea rushwa"
alisema Sisiwaya
Aidha katika hatua nyingine Kamanda Sisiwaya
alisema, pamoja na changamoto zilizopo, jeshi la polisi Pwani
limejipanga kukomesha ajali zote za barabarani zinazosababishwa na
uzembe na ulevi wa madereva wakati wakiendesha.
Alisema kipindi
cha sikukuu ya Krismas na mwaka mpya, ajali nyingi hutokea, lakini
katika kipindi cha sikukuu hizo musimu huu, walidhibiti vyanzo vyote vya
ajali hizo kiasi kwamba hakuna akali hata moja iliyotokea ndani ya mkoa
wa Pwani katika kipindi chote cha sikukuu ya krismas na mwaka mpya.
No comments:
Post a Comment