Bunda
MAISHA ya mtoto mwenye umri wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la tano, shule ya
msingi Bwanza (jina tunalo), wilaya ya Bunda mkoani Mara yako hatarini baada ya
samaki aina ya sato kumrukia na kuingia tumboni mwake kwa kupitia sehemu yake
ya siri.
Tukio hilo la aina yake, lililowashangaza wengi kijijini hapo na maeneo
mengine jirani, lilimtokea mtoto huyo Januari mosi, mwaka huu, saa 11 alfajiri
alipokuwa amechuchumaa akiteka maji ndani ya ziwa Victoria kwa lengo la
kumwagilia bustani yao ya nyanya na vitunguu waliyoilima kandokando ya ziwa
hilo.
SOMA ZAIDI…
Akiwa amechuchumaa akiteka maji, samaki huyo anayedaiwa kuwa mwenye ukubwa wa
nchi nne, aliruka kutoka majini na kumuingia sehemu yake ya siri na kuzama
kabisa tumboni mwa mtoto huyo ambaye, jitihada zake za kumvuta ili
asizame tumboni hazikufua dafu kwani aliambulia maumivu makali na kutokwa na
damu nyingi sehemu yake ya siri kwa kuparazwa na miiba ya mgongoni ya
samaki huyo.
Baada ya tukio hilo, alirudi nyumbani kwa shida, akijivuta na kuugulia maumivu
makali na kumweleza mama na ndugu zake mkasa uliomkuta ambao,
walimchunguza na kujaribu kuingiza mkono sehemu yake ya siri wakidhani
watampata samaki huyo lakini hawakufanikiwa.
Kaka wa mtoto huyo, Lenatus Mtani (31) alisema, walipompeleka katika zahanati
iliyopo kijijini hapo, hali yake ilizidi kuwa mbaya, akilalamika maumivu makali
tumboni, ndipo familia akalihusisha tukio hilo na imani za kishirikina na
kuamua kumtoa katika zahanati hiyo na kijijini hapo, na kumpeleka kwa mganga wa
kienyeji katika kijiji cha Amuyebe, wilayani Ukerewe.
"Mdogo wangu amechezewa kamchezo, katika hali ya kaawaida samaki hawezi
kumrukia mtu sehemu yake ya siri na kuzama tumboni, huu ni ushirikina,
tumempeleka kwa mtaalamu lakini bado hali yake inazidi kuwa mbaya" alisema
Bw. Mtani
Alisema hata baba yao alifariki katika mazingira ya utatanishi mwaka 2003,
kisha kaka zake watatu nao wakafariki kwa mfululizo mwaka 2004, 2005, 2006 wote
hao vifo vyao vikigubikwa na utata akidai ni kutokana na ugomvi wa shamba uliopo
kati ya familia yao na mkazi mmoja wa kijijini hapo.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Alwego anakoishi mtoto huyo, Bi. Reticia Bituro
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo alilodai limemshutua na kumshangaza sana
kwani, hajawahi kushuhudia tukio la namna hiyo tangu azaliwe na kuahidi
serikali yake kulifanyia uchunguzi wa kina ili kubaini kama ni mapenzi ya Mungu
au kuna mkono wa mtu.
Naye diwani wa eneo hilo la kata ya Napindi Bw. Elias Magoti ambaye yuko safari
kuhudhuria kikao cha baraza la madiwani Bunda mjini alikili kupokea taarifa za
tukio hilo kwa mshangao mkubwa na kudai atalifuatilia kwa karibu atakaporudi
kijijini kwa kufanya uchunguzi kubaini kilichotokea kwani hajawahi kusikia
tukio la namna hiyo katika umri wake wote.
Taarifa zilizopatikana kutoka ukerewe anakotibiwa mtoto huyo, zilisema hali
yake inazidi kuwa mbaya, hawezi kuzungumza na anazidi kulalamika maumivu makali
tumboni ikielezwa kwamba, samaki huyo bado yumo tumboni mwa mtoto huyo.
No comments:
Post a Comment