Thursday, January 09, 2014

NJEMBA YAKAMATWA NA BUNDUKI NA NDEGE

Singida

Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Agustino Lorry (43) amekamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kupatikana na Bunduki mbili na ndege hai 12 aina ya Flamingo vyote vikiwa nyumbani kwake.

Bunduki hizo mbili moja aina ya Riffle V. 15152 na Shotgun No. 729 na Nyaraka hizo za serikali vilipatikana nyumbani kwake katika maeneo ya Sabasaba Kata ya Mandewa mjini Singida.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishina Msaidizi Mwandamizi Geofrey Kamwela , siku ya tukio Jeshi hilo lilipata taarifa za siri kutoka kwa raia mwema kuhusu mtuhumiwa kujihusisha na vitendo vya usafirishaji wa ndege.

Akizungumza na waandishi wa Habari juzi Kamanda Kamwela alisema kuwa taarifa hizo pia zilibainisha kuwa Agustino Lorry alikuwa na ndege wengine nyumbani kwake wa aina ya Flamingo.

“Askari Polisi walimpekuwa nyumbani kwake, na kukutwa akiwa na silaha hizo mbili pamoja na Risasi tatu mbili za shortgun na moja ya Riftle, vyote vikiwa vimefichwa chumbani kwake chini ya godoro la litanda chake” alisema Kamwela.

Alieleza kuwa hata hivyo upekuzi huo ulipokuwa unaendelea katika mazingira ya nyumba ya mtuhumiwa ndege hao walikutwa wamefichwa katika chumba kimoja cha uani.

“Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa ndege hao waliletwa kwa Lorry na mtu mwingine anayedaiwa amekuwa akishirikiana naye na ndiye mtegaji na ukamataji wa Nyara hizo za Serikali.” Alisema Kamanda huyo.

Aliongeza kuwa Jeshi hilo lilishirikiana na Idara ya wanyama pori Mkoani hapa kufuatilia tukio hilo na kufanikiwa kumkamata mtu mwingine Hamza Ally(40) Mkazi wa Mtaa wa Majengo mjini Singida.

“Alikutwa katika Ziwa Singidani lililopo mjini hapa akiwa katika harakati za kutega na kukamata ndege wengine kwa lengo la kusafirishwa”.alisema Kamanda huyo.

Alieleza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ikiwa ni pamoja na kujua wamiliki halali wa Bunduki hizo, na jinsi zilivyofika kwa mtuhumiwa Agustino Lorry ambaye ni mfanyakazi wa Serikali.

Jeshi la Polisi Mkoani Singida limetoa tahadhari kuwa litashirikiana na Idara hiyo pamoja na wananchi ili kudhibiti vitendo vya ujangiri ambavyo vimekuwa vikitishia kumalizika kwa wanayama pori na ndege hapa Tanzania

No comments:

Post a Comment