Friday, December 20, 2013

UKATILI WA KUTISHA:WATOTO WAWILI WACHINJWA NA KUNYONGWA

Watoto wawili wa Diwani Chama Cha Mapinduzi (CCM)wa kata ya Mkangamo Eston Kimwelu wameuwawa kikatili na wananchi wenye hasira kwa kuwanyonga na waya kisha kuwachinja shingoni kwa kisu .

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi, Barakael Masaki alisema kuwa tukio hilo limetokea Desemba 19 mwaka huu saa 8.00 mchana katika eneo la TAZARA Tunduma katika Wilaya ya Momba.

Alisema kuwa watoto waliouwawa kinyama ni pamoja na Kalibu Kimwelu(6) ambaye aliuwaa kwa kuchinjwa shingoni na kundi la watu wasiofahamika walioingia nyumbani kwa diwani huyo na kufanya unyama.

Kamanda Masaki alisema kuwa wauwaji hao baada ya kufanya unyama huo walimnyonga msichana wa kazi aitwaye, Sista Nyilenda (17) wakati tayari wameshafanya tukio la kinyama la mtoto Kalibu.

Hata hivyo Masaki alisema wauwaji hao wakati wakitekeleza azma ya kufanya unyama huo walichukua waya wa Tv uliokuwepo sebuleni kisha kumnyonga nao binti huyo.

Aidha Kamanda huyo alisema kuwa mbinu iliyotumika kwa wauwaji hao ni kuwavamia wahanga wakiwa ndani nyumba waqkiwa wamekaa sebuleni .

“Baada ya kufanya unyama huu wauwaji hawa waliondoka na kuacha miili hiyo ikiwa sebuleni wakati wazazi wa watoto hao wakiwa hawapo nyumbani “alisema Kamanda Masaki.

Hata hivyo Masaki alisema wakati tukio hilo linatokea Baba na Mama wa Mtoto huyo ambapo baba ni ,Diwani CCM ,Eston Kimwelu (55) alikuwa katika kijiji cha Kipaka ambako ana mashamba yake na Mkewe aitwaye Tumaini Yohana (29)ambaye ni katibu muhtasi halmashauri ya mji mdogo wa tunduma alikuwa kazini.

Aidha Kamanda Masaki alisema kuwa watu hao baada ya kufanya mauaji hayo pia waliiba mabegi makubwa mawili yenye nguo mbalimbali yaliyokuwa katika chumba wanacholala watoto hao.

Akizungumzia kuhusu mazingira ya tukio hilo Masaki alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo kinachunguzwa ingawa uchunguzi wa awali unaonyesha ni mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia kati ya mke mkubwa na mdogo kufuatia familia ya mke mkubwa kudai kutelekezwa na kunyimwa mali/mashamba.

Alisema kuwa katika tukio hilo watuhumiwa watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambao ni ,Gabriel kimwelu (19) Enock Simwelu(23)Alex Simwelu (16) mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari mpakani wote ni watoto wa mke mkubwa wakazi wa Majengo Mapya Tunduma.

Wengine ni Mussa Ngoba (19)mkazi wa mtaa wa mwaka tunduma pamoja Patrick Msigwa,(18) mkazi wa majengo ambao majirani na marafiki wa watoto hao.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika kituo cha afya cha Tunduma kwa uchunguzi zaidi ili iweze kukabidhiwa kwa ndugu .

Kaimu Kamanda huyo alitoa wito kwa wazazi/walezi kuzingatia suala la malezi bora kwa watoto na vijana wao ili wakue katika maadili mema na kujiepusha na matukio ya uhalifu na kusisitiza kuwa na taifa lenye ustawi mzuri wa jamii suala la malezi bora kwa watoto ni jukumu la kila mtu .

Masaki ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali walipo watu waliohusika na tukio hilo wazitoe katika mamlaka husika ili wakamatwe na hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe.

No comments:

Post a Comment