Friday, November 08, 2013

KOCHA WA AZAM ATIMULIWA

Huku ligi kuu soka Tanzania Bara ikiwa imekamilisha mzunguko wake wa kwanza hii leo,timu ya Azam FC ya Dar es Salaam imetangaza kusitisha mkataba na kocha wake mkuu Stewart Hall (Pichani Kushoto) wa Uingereza kwa kile kilichoelezwa kama makubaliano ya pamoja.

Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa klabu hiyo jijini Dar es Salaam, hii itakuwa ni mara ya pili kwa kocha huyo kuachana na klabu ya Azam na ameafikiana na uongozi wa klabu hiyo baada ya kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ambapo timu ya Azam sasa inashika nafasi ya Pili baada ya kwenda sare ya mabao 3-3 na timu ya Mbeya City ambapo zote sasa zina Pointi 27. Bingwa mtetezi timu ya Yanga inaongoza ligi hiyo kwa sasa ikiwa na pointi 28 baada ya kuinyuka Oljoro JKT mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, maaruf kama Vodacom Premier League.

Klabu ya Azam FC inayoinukia kwa ubora wa miundo mbinu huku ikiendeshwa kisasa kwa mipango inayoeleweka kinyume na klabu nyingi nchini Tanzania imekuwa ikifanya vema chini ya mwalimu huyo ambapo msimu uliopita aliiwezesha kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kushika nafasi ya Pili katika Ligi kuu msimu uliopita.

Klabu hiyo inao wachezaji kadhaa wa Kulipwa kutoka nchi za Ivory Coast, Kenya na Uganda. Kuachia ngazi kwa kocha huyo kunaelezwa kuwa kumekuwa kwa mkakati ili kusiathiri mwenendo wa timu hususan wakati ligi ikiendelea na sasa kutaiwezesha Azam FC Kutafuta kocha mwingine hususan wakati huu ambapo ligi imefikia mapumziko.

No comments:

Post a Comment