Sunday, July 28, 2013

WATANZANIA WAKAMATWA NA DAWA ZA KULEVA HONG KONG


WATANZANIA watatu wanadaiwa kukamatwa nchini mjini Hong Kong nchini China  wakisafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya sh. bilioni moja. Dawa hizo zimetipotiwa kuhifadhiwa katika kitengo cha madawa ya kulevya nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa serikali ya Hong Kong, maofisa wa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Hong Kong(HKIA) walimkamata kijana wa miaka 26 ambaye ni abiria kutoka Tanzania juzi mchana akiwa amebeba kilo 1.6 za dawa aina ya heroine zikiwa kwenye sanduku lake la mkononi (briefcase).


Dawa hizo (picha ndogo juu kushoto) zinadaiwa kuwa na thamani ya ya sh. milioni 270. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo siku hiyo hiyo jioni maofisa wa ushuru tena walimkamata mtu wa miaka 45 akitokea Tanzania. Mtu huyo alikamatwa akihisiwa kuwa amebeba dawa mwili mwake (picha ndogo kulia juu).

Mtuhumiwa huyo alipelekwa hospitali na kutolewa dawa hizo zenye uzito wa gramu 204 aina ya heroine zenye thamani ya sh. milioni 35. Kwa mujibu wa taarifa hizo mtuhumiwa huyo bado yuko hospitali.

Habari zaidi zilieleza kwamba siku hiyo hiyo maofisa hao tena walimkamata mtu mwingine mwenye umri wa miaka 28 akiwa katika eneo la maegesho ya magari ya Tai Kok Tsui akiwa na dawa aina ya kokaine yenye uzito wa kilo 2.03 zilizokuwa zimebebwa na kuhifadhiwa kama vitafunwa ndani ya mfuko wa plastiki aliokuwa amebeba (Picha za chini pichani).

Maofisa hao walimpeleka kijana huyo katika jengo lililokuwa karibu na maegesho hayo na baada ya kupekuliwa alikutwa na kilo moja ya dawa aina ya Kokein zenye thamani ya sh. milioni 700.

Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza majina ya watuhumiwa hao wala utaifa wa mtuhumiwa wa tatu. Msemaji wa idara ya ushuru katika uwanja huo alisema watu hao watashtakiwa kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya. Uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa.

Taarifa hiyo ilionesha picha tatu za dawa hizo zilizopo pichani kushoto zikionesha jinsi zilizovyokuwa zimehifadhiwa.

Kwa sheria za Chini mtu yeyote akikamatwa dawa za kulevya adhabu yake ni kifungo cha maisha pamoja na faini ya dola za HongKong milioni 5.

Mwandishi wa habari hii lilipowasiliana na Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Geofrey Nzoa, kuhusiana na taarifa hizo, alisema taarifa hizo bado hawajazipata nchini na kwamba wanajaribu wanawasiliana na wahusika nchini China.

Alisema kwa sasa wanajaribu kuangalia walitumia usafiri gani kwenda huko. Kama ni ndege, alisema wataenda kwenye shirika la ndege ambalo wamesafiri nalo ili kujua majina yao.



No comments:

Post a Comment