Monday, July 22, 2013

MJANE ATIMULIWA NJE



Hata kabla ya maziko askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa Darfur, Sudan hayajafanyika, mchumba wa mmoja wa wapiganaji hao, Amina Juma ameonja chungu nyingine baada ya kutimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu mwenza wake.

Amina ambaye inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na Fortunatus Msofe aliyekuwa askari katika Kambi ya Msangani, 36KJ Pwani alisema jana: “Kumekuwa na mzozo wa hali ya juu na ndiyo maana tumeshindwa hata kufika Uwanja wa Ndege kuupokea mwili na hata kesho (leo) sidhani kama nitakwenda... kuna mtafaruku mkubwa wa kifamilia.”


Baada ya kutimuliwa, Amina ambaye hawakuwahi kupata mtoto na marehemu Msofe, alilazimika kuondoka kwenye nyumba hiyo na kwenda Mlandizi kwa wazazi wake. “Nimeishi na Msofe kwa miaka mitatu, akiwa kambini mimi niko hapa na wakati mwingine alikuwa analala huku... lakini leo wamenitimua,” alisema huku akilia.

Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.Ilidaiwa kwamba Amina alitimuliwa katika nyumba hiyo Ijumaa iliyopita, saa saba mchana baada ya ndugu watatu wa marehemu kufika hapo wakitokea Tanga.

Walipofika inadaiwa kuwa walitangaza kusitishwa msiba huo katika nyumba hiyo na kutangaza kutomtambua mke huyo. Watu hao waliwaeleza waombolezaji kuwa walitumwa na baba mzazi wa marehemu, Willbad Msofe kutoka Kange, Tanga kufika Kibaha kusitisha msiba uliokuwa ukiendelea nyumbani kwa mtoto wake huyo.

Inadaiwa pia kuwa katika msafara huo, alikuwapo mdogo wa marehemu ambaye aliwahi kuishi kwa miaka miwili na Amina hapo Visiga. Ilidaiwa kuwa walipofika nyumbani hapo walionana na mfiwa, Amina na wazazi wake ambao pamoja na majirani na watu wengine wengi, walikuwa wakimfariji binti yao huyo.

Mmoja wa waombolezaji alisema baada ya salamu wanandugu hao walianza kuulizia mali za marehemu na walikuwa wakimuuliza Amina ambaye aliwaleza kila kitu kilipo na baada ya hapo ndipo walipomweleza kuwa wametumwa na baba wa marehemu kuwa watu hawatakiwi kuomboleza kwenye eneo hilo kwani msiba upo Tanga tu ambako ndiko iliko familia yake.

Alipoulizwa baba wa marehemu, Mzee Msofe alisema: “Mimi ndiye niliyeagiza nyumba ifungwe na ukweli ninamfahamu Amina, lakini simtambui kama mkewe kwa kuwa hawajafunga ndoa... Hata wewe si unayafahamu haya? Uchumba si ndoa na ukifunga ndoa ndipo unatambulika rasmi,” alisema.





No comments:

Post a Comment