Tuesday, June 11, 2013

KIKOSI CHA UTALII NCHINI CHAPATA KAMANDA MPYA

 Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Aloyce Nzuki, akimkaribisha Kamanda wa Kikosi kipya cha Utalii cha Jeshi la Polisi, Kamishina Msaidizi (ACP), Maria Nzuki (kushoto). wakati wa mkutano wa kumtambulisha kwa viongozi wa bodi hiyo uliofanyika Dar es Salaam jana.

Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Utalii cha Jeshi la Polisi Kamishina Msaidizi (ACP), Maria Nzuki, ameahidi kushirikiana na wadau wa utalii katika kuhakikisha usalama wa watalii
wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Akizungumza wakati wa hafra maalumu ya utambulisho kwa viongozi mbalimbali wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dar es Salaam jana, mkuu huyo alisema jeshi la polisi nchini litahakikisha usalama wa wageni wanaotembelea vivutio mbalimbali wanakuwa salama na mali zao.

'Tumejipanga kikamilifu kusimamia usalama wa wageni wetu na hilo litawezekana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo wamiliki wa hoteli na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na sekta hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu',

Pia aliongeza kuwa jeshi hilo haliwezi kufanya kazi peke yake lazima lishirikiane na wadau na wananchi ili kutimiza malengo yalikusudiwa kuwepo kwake hivyo ushirikiano utasaidia kupatikana kwa taarifa mbalimbali za kiusalama katika maeneo ya mbuga za wanyama na vivutio vingine.

Naye Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki, alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema kwa uamuzi muafaka wa kuanzisha kikosi hicho ambacho ana uhakika kitasaidia kuimarisha usalama na kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini.

Aliongeza kuwa bodi yake itakuwa ikiindaa makongamano ya wadau ili kukiwedhesha kikosi hicho kuwafahamu wadau wa utalii na mahitaji yao ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mkurugenzi huyo alizitaja baadhi ya nchi zilizofanikiwa katika masuala ya utalii na usalama wa watalii kwa kutumia vikosi maalumu nchi hizo ni Zimbambwe, Misri na Mauritius

Alisema juhudi zinazoendelea za kutangaza vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani umesaidia kuongeza watalii waliotembelea Tanzania kutoka 860.000 na kufikia zaidi ya milioni 1.1 katika kipindi cha 2011 hadi 2012 na juhudi zinafanyika ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu zikiwamo hoteli na usafiri wa uhakika katika hifadhi zetu.

Kuundwa kwa kikosi hicho kipya ambacho kitasimamia usalama katika maeneo yote ya utalii nchini kama vilivyo vikosi maalumu vya reli na Bandari kutaongeza imani kwa watalii kutembelea mbuga na vivutio mbalimbali bila hofu ya usalama wao.




No comments:

Post a Comment