Thursday, June 07, 2012

SAKATA LA ATCL:KIBAO CHAMGEUKIA WAZIRI MWAKYEMBE


Na mwandishi wetu

WAFANYAKAZI wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), wamefikisha kilio chao kwa baadhi ya wabunge wakipinga hatua ya Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, kutengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Paul Chizi, wakidai hatua hiyo inatokana fitina, iliyotengenezwa dhidi yake.

Wafanyakazi hao walienda mbali wakisema kuwa hali hiyo kama itaendelea, itamnyima uhuru wa kufanyakazi kazi Kaimu Mkurugenzi Mpya, Kapteni.Lusanjo Lazaro na wafanyakazi wa chini yake kwa ujumla.

Baadhi ya wafanyakazi wa ATCL walifikisha kilio chao kwa wabunge waliosafiri na ndege ya shirika hilo jana aina ya Boing  737-500  iliyokuwa ikisafiri kutoka Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya kuaminika kutokana ndani ya ndege hiyo wabunge waliofikishiwa kilio hicho ni  Mbunge wa Nzega Bw. Hamisi Kigwangalla, Bw.John Cheyo (Bariadi Mashariki) Bw. Kanji Lugola (Mwibale), Bw. Vicent Nyerere (Musoma Mjini) na Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Nyamagana Bw. Emmanuel Mzungu na viongozi  wengine wa Serikali.

"Bw. Chizi alikuwa akinyimwa ushirikiano na uongozi wa Wizara ya Uchukuzi, kiasi kwamba hata wakati ndege hiyo inawasili kuanza safari nchini hakuna viongozi wa juu walioenda kuipokea," kilisema chanzo chetu.

Kwa mujibu wa watoa habari hizo, ilielezwa kuwa chuki dhidi ya Bw. Chizi zilianza tangu awali alipositisha utaratibu wa ndege za shirika hilo, kwenda kufanyiwa matengenezo nje ya nchi na badala yake yakaanza kufanyika nchini, ambapo sasa ndege yake nyingine ipo hatua za mwisho.

"Uamuzi wake huo ulionekana kugusa maslahi ya baadhi ya viongozi waliokuwa wakinufaika na utaratibu huo wa ndege kutengenezwa nje," alisema mmoja wa wabunge akinukuu mmoja wa wafanyakazi wa ndege hiyo.

Walidai kitendo cha Waziri wa Uchukuzi. Dkt.Harrison Mwayembe, kutengua uteuzi wa mkurugenzi huyo kwa madai kuwa uteuzi wake haukufuta sheria na kanuni za utumishi wa umma ni za fitina.

"Tunajua kuwa kuliwapo na fitina tangu mwanzo na ndiyo maana hata katika uzinduzi wa ndege hii hakuna kiongozi kutoka wizarani aliyefika," alisema mmoja wa wafanyakazi katika ndege hiyo.

Walidai kuwa Waziri Mwakyembe hakupaswa kuchukua uamuzi huo haraka, kwani ilitakiwa kuchunguza kabla ya kutengua uteuzi wake.

Wafanyakazi  hao waliwaeleza wabunge kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mkurugenzi huyo kuenguliwa kwa sababu ya juhudi zake za kuziba mianya ya ubadhirifu, lakini Dkt. Mwakyembe bila kujua alijikuta akifikia uamuzi wa kumsimamisha bila kuchunguza.

"Ilitakiwa kabla ya waziri kuchukua hatua hiyo kwanza angeangalia utendaji wake, kwani tangu aingie madarakani amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadilisha hali ya shirika tofauti na awali," alinukuliwa akisema mmoja wa wafanyakazi wa ndege hiyo akiungwa na baadhi ya abiria.

Watumishi hao walidai kuwa kati mianya ambazo amefanikiwa kuziba ni kuacha kutengeneza ndege nchini Urusi, ambapo kwa sasa zinatengenezwa kwenye karakana ya ATCL nchini.

"Tunasema kilicho cha kweli huyu mkurugenzi alitumia nguvu zake kuhakikisha kuwa ndege hizo zinafanyiwa matengenezo hapa nchini, pia aliweza kupunguza gharama za nauli na kuwa bei tofauti na ndege za mashirika mengine hilo ndilo lililomsababishia watu kumchukia wakiwemo viongozi wa mashirika ya ndege mengine ambao hawaitakii mema ATCL," alisema mmoja wa watumishi wa ndege hiyo huku wakionekana kukosa raha tofauti na zamani.

Mbunge wa Musoma Mjini,Bw. Nyerere alikiri kupokea malalamiko hayo, ambayo yameonesha wazi kuwa hawakufurahishwa na uamuzi wa waziri.

"Ndani ya ndege hiyo tulikuwa wabunge wengi na tulikuwa tukitokea kwenye mkutano wa Bodi ya Pamba, mkoani Mwanza ndipo tulifikishiwa kilio chao...nina imani malalamiko hayo yatasikilizwa," alisema mbunge huyo.




No comments:

Post a Comment