Tuesday, March 20, 2018

MAJALIWA AFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA MASUALA YA AFYA

PICHANI: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa kimataifa wa masuala ya Afya, uliohudhuliwa na Mawaziri kutoka nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya kati na Afrika ya Kusini.

Na WAMJW. 
Dar es salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaaliwa afungua Mkutano wa 65 wa Mawaziri wenye dhamana ya Sekta ya Afya katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (Eastern, Central and Southern Africa Health Community, (ECSA HC)

Katika ufunguzi huo Waziri Mkuu amewataka wananchi wanachama wa Jumuiya hiyo kufuata mtindo bora wa maisha pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo hivi sasa unaongezeka kwa kasi na kupelekea vifo kwa jamii.

Mhe. Majaliwa aliendelea kusema kuwa ajenda ya mwaka 2030 ni kutomuacha mtu nyuma katika kupambana dhidi ya magonjwa ili kurahisisha utekelezaji azma ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga Tanzania ya uchumi wa viwanda.

Aidha,alisema jumuiya hiyo inatakiwa kuhimarisha ushirikiano hasa katika masuala ya Sekta ya Afya ili kuweza kusaidiana katika kutatua changamoto zinazoikumba Sekta hiyo baina ya mataifa hayo.

“kumekuwepo na magonjwa ya mlipuko hasa kwenye maeneo ya mipakani kama vile ebola,kipindupindu na mengineyo hivyo mkutano huu utaleta tija na kupata njia ya kuondokana na magonjwa haya na kutimiza malengo endelevu ya afya kufikia mwaka 2030”.

Waziri Mkuu alitaja maeneo ambayo mkutano huu umejikita ikiwemo ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto kuu nne (4) ambazo ni: Uongozi na Utawala bora katika Sekta ya Afya; changamoto za magonjwa ya kuambukiza; tishio la magonjwa yasiyoambukiza; na kuimarisha uwajibikaji katika afya ya mama na mtoto.

Mkutano wa Mawaziri wa afya wa Jumuiya hiyo inajumuisha Mataifa tisa (9) wanachama ikiwemo Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Lesotho, Zimbabwe, Swaziland, Mauritius na mwenyeji Tanzania.

Jumiya hii ilianzishwa mwaka 1974 ikiwa na lengo la kujenga ushirikiano wa kikanda na uwezo wa kukabili changamoto za sekta ya afya kwa kukuza ufanisi na ujuzi katika sekta ili kutatua changamoto zinazokumba wananchi.

Mada kuu ya Mkutano wa mwaka huu ni “Multisectoral collaboration for Health towards achieving the SDGs”, ikilenga kujenga uwezo na mshikamano kwa kushirikisha Sekta mbalimbali na wadau ili kuharakisha kufikiwa malengo endelevu ya afya (Sustainable Development Goals (SDGs) ifikapo mwaka 2030. 

Mkutano huu unafanyika kwa siku tatu katika Hotel ya Hyatt Regency, the Kilimanjaro, Dar es Salaam na umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ECSAHC.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (wakatikati) akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wakwanza kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya (wa mwisho kulia), wakiwa katika kikao cha kimataifa cha masuala ya Afya ambacho kimejumuisha nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya kati na Afrika ya Kusini, kikao hicho kimefanyika jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimsalimia moja kati ya Wadau wa afya baada ya kumaliza kikao cha kimataifa cha kujadili masuala ya Afya kilichofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimtembeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika banda la Bohari ya Dawa (MSD) mda mchache baada ya kumalizika kwa Mkutano wa kimataifa wa masuala ya Afya uliofanyika jijini Dar es salaam. (Picha zote na Wizara ya Afya)

No comments:

Post a Comment