TAMKO LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA TIBA YA ASILI YA MWAFRIKA
Ndugu wananchi,
Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yalianza rasmi mwaka 2003 baada ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika kuridhia kuwepo kwa sherehe hizo. Maadhimisho haya hufanyika katika nchi 46 za kanda ya Afrika ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani tarehe 31/08 ya kila mwaka.
Ndugu wananchi,
Tanzania, inaadhimisha maadhimisho haya kwa malengo makuu manne. Kwanza Tanzania ina nia ya kufufua ari na kujenga heshima ya huduma za tiba asili ambazo historia inatuambia kuwa zimekuwa zikikandamizwa na kudharaulika. Kwa kiwango kikubwa ukoloni pamoja na ukoloni mambo leo umekuwa ukikandamiza tiba zetu za asili na kufanya Waafrika wenyewe kuzinyanyapaa tiba hizo. Hali hiyo imetufanya tuyumbe, tukose dira na mwelekeo katika suala zima la kuboresha Tiba Asili katika nchi yetu.
Pili kwa kupitia maadhimisho haya Serikali inawahamasisha Waganga wa Tiba Asili kujiepusha na migongano katika jamii kwa kutohusisha ushirikina na uchawi kama chanzo cha ugonjwa. Kuna taarifa na migongano mingi ya kutisha juu ya hili. Itakuwa jambo la busara kwa waganga wa tiba asili kupitia kwenye vyama vyao kupanga mikakati ya kudhibiti na kuondoa kabisa vitendo vibaya vinavyochafua taaluma yao.
Tatu, maadhimisho haya yanahimiza masuala ya uboreshaji na usajili wa dawa za asili. Lengo ni kuweza kutengeneza dawa kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya utengenezaji dawa bora. Aidha utafiti endelevu wa dawa za asili kwa magonjwa mbalimbali unahimizwa kwa madhumuni ya kupata dawa ambazo zinaweza kupatikana kiurahisi ili mwenye kuhitaji aweze kuzipata.
Nne, kwa kupitia maadhimisho haya Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma na huduma za afya.
Ndugu wananchi,
Kama mnavyofahamu katika kuadhimisha Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika kila mwaka tunakuwa na ujumbe maalum au kauli mbiu. Ujumbe maalum wa mwaka huu ni “Ujumuishaji wa Tiba Asili katika Mifumo ya Afya: Tulipofika sasa” (“Integration of Traditional Medicine in Health Systems: The journey so far”).
Kauli mbiu hii inawalenga na kutoa majukumu kwa Viongozi na Wataalam wa Tiba ya Kisasa kuweza kushirikiana na Waganga wa Tiba Asili katika utoaji wa huduma za afya. Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inafanikiwa kuijumuisha huduma za tiba asili katika utoaji wa huduma za afya; Serikali imerasimisha huduma za tiba asili kwa kujumuisha katika Sera ya Afya; kuwepo kwa Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu za utoaji wa huduma za tiba asili nchini.
Aidha, Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kusajiliwa, kusajili vituo na dawa zao zinazotumika hususan dawa zinazouzwa katika maduka ya dawa za asili. Hadi tarehe 30 Juni, 2017; waganga 16,200; vituo 212 na dawa za asili tatu zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Huo ni mwanzo mzuri ijapokuwa juhudi zaidi zinahitajika kuwezesha “Ujumuishaji wa Tiba Asili katika Mifumo ya Afya: Tulipofika sasa”. Vilevile; nitoe wito kwa Waganga wa Tiba Asili kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zinazowasimamia katika kutoa huduma za tiba asili kwa wateja wao. Nawataka wajiepushe na matangazo yanayokizana na sheria, kanuni na taratibu ikiwa pamoja na kuondoa mabango yaliyozagaa mitaani yanayoonyesha kuwa wanaweza kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali kwa mfano UKIMWI.
Ndugu wananchi,
Napenda kuwakumbusha wananchi kwamba kwa sasa huduma za tiba asili zinatambuliwa rasmi kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Afya na Sheria namba 23 ya mwaka 2002. Madhumuni ya sheria hii ni kusimamia, kudhibiti na kuendeleza tiba asili ya Tanzania. Vilevile, udhibiti wa maadili ya uganga na ukunga wa tiba asili nchini umepewa kipaumbele.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala limeundwa kama chombo kikuu cha Serikali kitachosimamia na kuratibu shughuli hizo. Sheria hiyo pia inalinda afya na haki za watumiaji wa tiba ya asili na tiba mbadala, kuboresha na kuendeleza tiba na dawa za asili, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuondoa utoaji holela wa Tiba Asili. Ni muhimu kwa kila mganga wa tiba asili kuzingatia Sera, Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, kuachana na matangazo yasiyofaa, kuacha kuweka mabango hovyohovyo barabarani, matangazo katika vyombo vya habari ni lazima yapate kibali cha Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Ndugu wananchi,
Tanzania tunayo mitidawa mingi na mingi inayotumika kutibu magonjwa mbalimbali. Wataalam mbalimbali ikiwa pamoja na waganga wa tiba asili sajilini dawa zenu ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengi. Pia, ni ukweli usiopingika kuwa dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mitidawa, na elimu ya mwanzo kabisa juu matumizi ya miti hiyo kutumika kama dawa inatokana na waganga wa tiba asili. Tanzania ina rasilimali kubwa ya mitidawa na wapo waganga wenye ujuzi katika hilo. Hivyo basi, ni vyema waganga wa tiba asili kwa kushirikiana na Serikali kuendeleza ujuzi na utalaamu wao kwa madhumuni ya maendeleo yao na jamii nzima kwa ujumla.
Ndugu wananchi,
Mwaka huu 2017 maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika yanafanyika kwa kutoa elimu kwa wananchi kazi ambayo imeanza rasmi tarehe 28/08/2017 na itaendelea kutolewa hadi kilele tarehe 31/08/2017. Katika muda huo wote mada mbalimbali zitakuwa zinatolewa ili kuwaelimisha wananchi na hususan watoa huduma wa tiba asili na tiba mbadala kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo.
Wananchi na wadau wa tiba asili nchini ni vema mkasikiliza taarifa hizo.
Ahsanteni
No comments:
Post a Comment