Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia) akimsikiliza Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza (kulia), inayojenga barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa ameipa miezi minne Kampuni ya ujenzi ya Nyanza Road Works kuongeza kasi
ya ujenzi wa barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50
kukamilika kwa wakati na wananchi wa Kibondo na maeneo ya jirani kuweza
kuitumia.
Waziri Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo wilayani Kakonko
mkoani Kigoma mara baada ya kukagua barabara hiyo na kutoridhishwa na kasi ya
ujenzi wake. "Mwezi wa pili mwakani nitarudi hapa kukagua tena
maendeleo ya ujenzi wa barabara hii sababu bado kasi mnayokwenda nayo
hainiridhishi na kampuni hii ni ya kizalendo ambayo ilitakiwa kuwa ya
mfano", amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa amemsisitiza mkandarasi huyo kuzingatia
viwango bora vya ujenzi wa barabara kama ilivyosainiwa kwenye mkataba na
kumtaka kuzingatia thamani ya fedha katika ujenzi anaoufanya. "Rafiki yangu ni yule anayefanya kazi vizuri hata kama
awe mwanangu kama hafanyi kazi vizuri nitamfukuza", amesisitiza Waziri
Mbarawa.
Naye, Mkandarasi wa kampuni hiyo Bw. Atul Ramji ameahidi
kutii na kulifanyia kazi agizo la waziri huyo na kusema kuwa ifikapo mwezi wa
pili mwakani ujenzi utakuwa umepiga hatua kubwa.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),mkoa
wa Kigoma Eng. Narcis Choma amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa sasa umefika
asilimia 18 kutoka asilimia tano zilizokuwepo awali ambapo kwa sasa kazi
zinazofanyika ni ujenzi wa makalvati katika barabara hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amemuagiza mkandarasi
wa kampuni hiyo kuanza mara moja kuipatia huduma ya maji Shule ya Sekondari ya
Kanyonza angalau mara moja kwa wiki kutoka kwenye kambi ya ujenzi wa barabara
wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu.
Prof. Mbarawa amechukua hatua hiyo baada ya wananchi wa
kijiji cha Kanyonza kumsimamisha na kumueleza changamoto ya Shule ya
Sekondari hiyo iliyopo katika kijiji hicho wilayani Kakonko kukabiliwa na uhaba
wa maji hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilometa nne
kufuata huduma hiyo.
Imetolewa na kitengo
cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment