TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepiga marufuku
uharibifu mkubwa wa mazingira unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambao
unaweza kusababisha nchi kugeuka jangwa.
Makamu wa
Rais ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kufungua mkutano kimataifa unaohusu mabadiliko ya tabia ya nchi unaokutanisha
wanasayansi, watafiti na wadau wa mazingira chini ya Usimamizi wa Kigoda cha
mwalimu Julius Nyerere cha Mazingira na mabadiliko ya Tabia ya nchini katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Makamu wa
Rais ameonya kuwa jukumu la kuhifadhi mazingira sio la Serikali peke yake bali
ni kila mwananchi na wadau wa mazingira kwa ujumla, hivyo wananchi ni muhimu
kwa umoja wao wakaongeza jitihada za kupanda miti katika maeneo yao ili
kukabiliana na hali tete ya uhabifu wa mazingira nchini.
“Uharibifu wa mazingira usimame leo
na marekebisho ya uharibifu tulioufanya uanze leo na hili ni jukumu la kila
Mtanzania”
Makamu wa Rais
pia ametoa wito maalum kwa viongozi wa ngazi zote nchini kuchukua hatua katika
kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji katika maeneo yao ili visitoweke.
Makamu wa
Rais ametahadharisha kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yameanza kuleta athari si
kwa Tanzania na dunia kwa ujumla hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili
kuhakikisha changamoto zinazojitokeza kwa sasa zinakabiliwa ipasavyo.
Kwa upande
wake,Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya mabadiliko ya Tabia ya nchi,Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam Profesa Pius Yanda amesema mkutano huo wa siku TANO utakuwa
na jukumu kubwa la kujadili kwa kina namna bora ya kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabia ya nchi.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam
31-Oct-2016
No comments:
Post a Comment