Na Mwandishi Wetu, Tanga.
Hatma ya mgogoro wa kiti cha umeya katika Halmashauri ya Jiji la Tanga yamalizika leo baada ya madiwani wa chama cha wananchi CUF kuingia kwa mara ya kwanza katika kikao cha baraza la madiwani na kukiri kumaliza tofauti iliyokuwepo sanjari na kufanya uchaguzi wa kuunda kamati za Halmashauri hiyo.
Hatimaye madiwani hao wameamua kumaliza tofauti zao zilizodumu kwa takribani mwaka mmoja kufuatia sakata la uchaguzi wa umeya uliosababisha kusimama kwa shughuli za kimaendeleo katika Halmashauri hiyo.
Kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika leo ni muendelezo wa vikao vingine vya baraza la madiwani vilivyokaliwa ambapo madiwani wa chama cha wananchi CUF hawakushiriki kutokana na kikao hicho kuvunjika.
Kikao cha leo ni muendelezo wa kikao cha tarehe 19 desemba mwaka jana ambapo waliingia katika tofauti baada ya Mkurugenzi wa jiji kutangaza nafasi ya umeya kuchukuliwa na chama cha mapinduzi ccm ambapo chama cha wananchi CUF hakikuridhika na matokeo hayo.
Awali akifungua rasmi kikao cha kwanza cha baraza la madiwani Mstahiki Meya wa jiji la Tanga Mustafa Selebosi alisema wameamua kuondoa tofauti zao na kuungana kwa pamoja ili waweze kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua sambamba na kufanya kazi za Halmashauri kwa pamoja ili kuliletea Jiji la Tanga maendeleo.
Selebos alisema wameamua kuangalia maslahi ya Tanga kwa kuondoa tofauti zao kwani kuanzia hivi sasa wanakwenda kutekeleza majukumu ya halmashauri ipasavyo kwa kufuata misingi kanuni na taratibu ili kuhakikisha wanafidia muda wote waliosimama katika kuwaletea wananchi maendeleo kutokana na mgogoro huo.
Aliwataka madiwani hao kufanya kazi kwa uadilifu na kusimamia kanuni ili kufikia malengo na kuepuka majipu madogomadogo huku akitaka ruzuku za serikali na fursa zilizotaka kuletwa Tanga zipelekwe kwa kuwa hivi sasa hakuna mgogoro tena wameamua kumaliza tofauti zao.
"Muda wa uchaguzi umepita ni wakati wa kuungana kwa pamoja na kushirikiana kwa kila hali ili tuweze kufanya mabadiliko makubwa katika jiji letu kwani Nchi nzima sasa imekuwa ikisubiri muafaka wa jambo hili upatikane naamini leo hii tumekuwa kitu kimoja tumeivisha nguo serikali wananchi mjivunie sasa kufanya kazi na Halmashauri yenu,"alisisitiza Selebos.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji la Tanga Daudi Mayeji aliwashukuru madiwani hao kwa kuamua kwa moyo mmoja kufanya kazi ya kuungana kwa pamoja ili waweze kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua katika maeneo yao.
Mayeji alisema kwa muda mrefu swala hilo limekuwa likiwapa wakati mgumu kutokana na vikao vya baraza kutokaliwa na kueleza kuwa viongozi wa serikali na vyama wamefanya kazi kubwa na nzuri ya kuwaunganisha madiwani hao sanjari na kumaliza tofauti hiyo.
Naye Mbunge wa jiji la Tanga kupitia chama cha wananchi CUF Mussa Mbaruku alisema madiwani ni jicho la serikali katika Halmashauri hivyo wanapaswa kutambua wajibu wao ili penye hitilafu warekebishane na kuwataka kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa nafasi aliyonayo ili Halmashauri iweze kupiga hatua.
"Tujue Halmashauri ni wananchi watendaji na madiwani bila umoja upendo na ushirikiano basi hakuna chochote kitakachofanyika hivi sasa maendeleo ya Tanga yatapatikana kutokana na fursa nyingi zinazokuja ikiwemo uwekezaji viwanda pamoja na bomba la mafuta tunapaswa kuelewa kidole kimoja hakivunjo chawa," alisisitiza Mbunge.
Alisema kufikia muafaka wa jambo hilo ni sahihi kwani maisha yanaendelea na kuwataka madiwani hao kufanya kazi kwa kujutuma bila kujali itikadi za vyama vyao ili kuhakikisha Halmashauri ya jiji la Tanga hairudi nyuma katika utendaji wake kwani ufanyaji kazi kwa bidii ndio utapelekea Halmashauri kutorudi nyuma.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Milapwa alisema amefurahishwa na kumalizika kwa mgogoro kwani hakuridhishwa na kazi za serikali kufanyika bila vikao vya madiwani kutokana na wao kutoa kauli nzito za shughuli zinazofanywa na Halmashauri na kuamini kuwa shughuli za maendeleo kwa wananchi ni kutokana na sauti za madiwani.
Katika kikao hicho waliteua kamati mbalimbali za Halmashauri ya jiji la Tanga kwa kuzingatia jinsia na itikadi za vyama ikiwemo kamati ya fedha na uongozi Alat, Maadili ya madiwani, Kamati ya kugawa viwanja, kamati ya ajira, kamati ya ukimwi, kamati ya mipango miji na mazingira, pamoja kamati ya uchumi afya na elimu.
No comments:
Post a Comment