Monday, July 04, 2016

MFALME WA AFRO POP 20 PERCENT ARUDI KWENYE GEMU NA SAUTI YA GHARAMA

Na Sultani Kipingo

Mfalme wa Afro Pop nchini Abbas Hamisi Kinzasa almaarufu kama 20% (Twenty per Cent) anavunja ukimya na kurejea kwa kishindo kwenye anga ya muziki, huku akiwa msanii wa kwanza kusaini mkataba na lebo mpya ya KOMBINENGA inayoendeshwa na producer nguli John Shariza a.k.a Mann Water.

PICHA: Producer nguli wa muziki nchini John Shariza a.k.a Mann Water (chini kushoto) akiweka saini kwenye hati ya mkataba wa lebo ya KOMBINENGA kurasimisha usimamizi wa kazi za msanii Abbas Hamisi Kinzasa almaarufu kama 20% (Twenty per Cent) akishuhudiwa na Wakili msomi Iddi M. Gogo wa Alpha Attorneys (juu kulia) aliyefanikisha zoezi hilo, pamoja na meneja uzalishaji wa Combination Sounds, Rowel Moses (juu kushoto) kwenye studio za Combination Sounds Kinondoni Studio jijini Dar es salaam.

Twenty Percent, ambaye mwaka 2011 alitwaa tuzo saba za Kilimanjaro Music Awards (KTMA) kwa mpigo, huku Mann Water akisomba tuzo mara mbili mfululizo za producer bora (mwaka 2013 na 2014), tayari amesharekodi vibao vitano na anatarajia kuachia ngoma moja mpya ya kwanza Julai 18, 2016, katika kuandaa albamu yake ya SAUTI YA GHARAMA.

"Nimerudi kuwachinja tena" anasema Twenty Per cent, akiwa anakamilisha kurekodi katika studio za Combination Sounds iliyoko Kinondoni Mkwajuni jijini Dar es salaam. "Nimerudi kurudisha sauti ya gharama kwa jamii. Sauti inayofundisha. Sauti inayoonya. Sauti inayoburudisha. Sauti inayozengua kila mtu, " anaogeza.

Tayari Tweny Per cent ameshasaini mkataba wa miaka mitano na lebo ya KOMBINENGA, katika hafla fupi iliyofanyika Jumapili katika ofisi za Combination Sounds. Kuanzia sasa shughuli zote za msanii huyu zitasimamiwa na lebo hiyo chini ya Producer Mann Water.

Wakili msomi Iddi M. Gogo wa Alpha Attorneys ndiye aliyefanikisha zoezi hilo la kutiliana saini mkataba lililoshuhudiwa pia na meneja uzalishaji wa Combination Sounds, Rowel Moses.

"Namkubali sana Twenye Pa kwani ni msanii aliyetimia na hutumii shuruba wakati wa kurekodi maana ana kipaji cha ajabu cha kutunga akiwa wima na kukariri hapohapo", anasema Mann Water, ambaye ameshafanya kazi na wasanii nyota kibao wakiwemo Lady Jay Dee, Ali Kiba, Ommy Dimpoz, Christian Bella, MB Dogg, Juma Nature, Mr Blue na wengine wengi.

Twenty Percent alitamba sana tokea mwaka 2006 kwa wimbo wake wa "Manemane" uliomfanya ashinde tuzo ya KTM, kabla ya kuweka historia ya kusomba tuzo saba kwa mpigo mwaka 2011. wakati huo nyimbo zilizompandisha chati zilikuwa ni "Tamaa Mbaya" na "Ya nini Malumbano" na "Maisha ya Bongo"

Mbali na Muziki Twenye Percent pia alitamba sana kwenye tasnia ya filamu ambapo alicheza kwenye mchezo uliofahamika kwa jina lake la 20%. Baada ya hapo akaamua kupumzika kwa muda na kujishugulisha na shughuli za kilimo. "Kilimo kinaendelea vyema na sasa nimeamua kurudi kwenye gemu ili kuwachinja tena" alimalizia, akiinuka kuelekea kwake Kimzichana, Mkuranga, Mkoa wa Pwani, anakoishi.



No comments:

Post a Comment