Tuesday, June 21, 2016

WACHAWI WAVAMIA MKUTANO WA INJILI JIJINI MWANZA

Na Binagi Blog_BMG

Katika hali ya kushangaza, binti mmoja (pichani katikati) ametoa ushuhuda mbele ya waumini wa Kanisa la EAGT Lumala Mpya lililopo Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza na kueleza jinsi alivyoshindwa kumtoa kafara mchungaji wa kanisa hilo, Dkt.Daniel Moses Kulola.

Ilikuwa katika Mkutano wa Open Your Eyes and See OYES 2016 uliomalizika jumapili iliyopita katika Viwanja vya Kanisa hilo, ambapo binti huyo anasema alitumwa na shangazi yake ili akamtoe mchungaji wa Kanisa hilo kafara lakini alipofika alishindwa kutekeleza adhma yake hiyo ovu.

"Baada ya kujipaka damu ya mnyama (hakutaja ni mnyama gani) nilibeba kitovu cha binadamu na kuja katika mkutano. Nilipojaribu kukukamata nilishangaa moto unatoka mdomoni mwako na kunichoma hivyo nikashindwa kukushika". Alisema binti huyo na kueleza kuwa walifikia maamuzi hayo kutokana na mchungaji huyo kukemea wachawi kila anapokuwa akihubiri.

Alisema baada ya kushindwa kumkamata mchungaji, Shangazi yake nae alifika katika mkutano huo na kujaribu kumshika mchungaji bila mafanikio na hivyo wakaamua kuhamishia mashambulizi kwa waumini wengine wawili wa kanisa hilo lakini nao wakaanza kutoa moto kama ilivyokuwa kwa mchungaji na hivyo zoezi lao kukwama.

Kutokana na maombi yaliyokuwa yakiendelea katika mkutano huo, nguvu za Mungu zilimzidia binti huyo na kushindwa kurudi nyumbani kwa njia ya kichawi (kupaa), ambapo alianguka chini na alipoamka akaanza kutoa ushuhuda wa adhima aliyokuwa nayo.

No comments:

Post a Comment