Frank Mvungi-Maelezo.
Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 inatarajia kufanya mapitio katika sheria mbalimbali ili kutoa mapendekezo yatakayowezesha kufanyika kwa marekebisho au kutungwa kwa sheria mpya kulingana na mahitaji ya sasa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na afisa Sheria wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. Hemed Lusungu wakati wa Mkutano na vyombo vya Habari uliolenga kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.
Akifafanua Lusungu amesema kuwa Sheria zitakazofanyiwa utafiti ili ziboreshwe na kuendana na Kasi ya Serikali ya awamu ya Tano ni sheria za uwekezaji (Review of the legal frame work Governing Investiment for viable economic growth).
“Tunataka sheria katika eneo la Uwekezaji ziendane na dhana ya mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli inayolenga kukuza viwanda vya ndani hivyo ni lazima tutazame eneo hili ili kuwa na sheria zitakayowezesha suala hili” alisisitiza Lusungu.
Akizungumzia mapitio katika sheria za Usafirishaji Lusungu amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na sheria zinazokidhi mahitaji ya sasa hivyo utafiti wao utatoa mapendekezo ili kulinda haki za wasafiri na wasafirishaji.
Alisema faida za Tafiti zinazofanywa na Tume hiyo ni kusaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea marekebisho ya sheria mbalimbali na pia kusaidia kutungwa kwa sheria mpya kulingana na mahitaji ya wakati akitolea mafano sheria ya Ununuzi wa Umma sura ya 410 .
Aliongeza kuwa sheria hiyo imekuwa ikilalamikiwa kurefusha mchakato wa manunuzi na kufanya bei ya bidhaa au huduma kuwa kubwa.
Kwa kuzingatia umuhimu wa Sheria hiyo Tume imeshafanya mapitio katika maeneo husika na kutoa mapendeklezo ambayo yataondoa kasoro zilizokuwepo awali.
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171.
Majukumu ya tume kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 4 (1),(2) na (4) Cha sheria ya Tume ni kufanya mapitio, utafiti na kutathmini maeneo au mfumo wa sheria husika na kutoa mapendekezo kwa Lengo la kuiboresha.
No comments:
Post a Comment