Thursday, May 12, 2016

BENKI YA KILIMO KUKOPESHA ZAIDI YA BILIONI 40 KWA WAKULIMA

Na Fatma Salum-MAELEZO

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imepanga kutumia zaidi ya shilingi bilioni 40 kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha mwaka 2016/17 hadi 2020/21 ambao umejikita katika kuhakikisha Tanzania inajenga uchumi wa viwanda na kuongeza kiwango cha ajira na uzalishaji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Thomas Samkyi (Pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.

Bw. Semkyi alisema kuwa Benki hiyo imeamua kusaidia utekelezaji huo ili kuwezesha upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini na kuleta mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ambao utachangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

“ Katika kuhakikisha tunaunga mkono Sera ya Kujenga Uchumi wa Viwanda nchini Benki ya Kilimo inatarajia kutoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa wakulima ambayo itakuwa ni ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu na kwa riba nafuu (kati ya asilimia 7 hadi 12 kwa mwaka).” Alisema Bw. Semkyi.

Aidha, Bw. Semkyi alifafanua kuwa mikopo hiyo inalenga kuwanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa kwa ajili ya kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara wa Benki hiyo Bw. Robert Pascal alisema kuwa kwa miradi mikubwa ya kilimo inayoendeshwa kati ya Serikali, Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, mikopo ya moja kwa moja itatolewa kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo hasa kuimarisha mifumo ya minyororo ya kuongeza thamani katika mazao ya kilimo.

Pia Bw. Pascal alieleza kuwa Benki hiyo itatumia bidhaa mbalimbali zenye ubunifu katika kuwezesha vikundi vya wakulima wadogo, wafugaji wa ng’ombe, samaki na kuku.

Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) imeanzishwa mwaka 2014 kwa madhumuni ya kutekeleza Sera za Serikali kuhusu upatikanaji wa fedha za kuendeleza kilimo.

No comments:

Post a Comment